Oct 05, 2021 23:43 UTC
  • Jumatano tarehe 6 Oktoba 2021

Leo ni Jumatano tarehe 29 Safar 1443 Hijria sawa na tarehe 6 Oktoba 2021.

Katika siku kama ya leo tarehe 29 Safar miaka 157 iliyopita, alifariki dunia Mulla Hussein-Ali Tuysirkani, msomi na alimu mkubwa wa Kiislamu katika mkoa wa Isfahani huko katikati mwa Iran. Alikuwa msomi mwenye maoni na mhakiki na alibobea sana katika elimu na taaluma kama fiqhi, na usulul fiqhi. Tuysirkani alijishughulisha na kufundisha na kuelea wanafunzi wengi kwa miaka mingi. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni Kashful Asrar chenye juzuu 11. Vitabu vingine vya mwanazuoni huyo ni Asul Aqaaid na Makarimul Akhaq.  

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni kusambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.

Kikao cha Sadat na makamanda wa jeshi la Misri tarehe 6 oktoba  

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 1981 maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walishambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Kizayuni sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri na nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo.

Picha ya mauaji ya Anwar Sadat

Na leo tarehe 6 Oktoba Misri ambayo ni moja kati ya tamaduni za kale zaidi duniani ilianzisha serikali ya jamhuri yenye bunge baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ina siku mbili za taifa ambazo ni tarehe 23 Julai na 6 Oktoba. Tarehe 23 Julai ni siku ya mapinduzi dhidi ya utawala wa kifalme wa mfalme Faruq hapo mwaka 1952 mapinduzi ambayo yaliandaa uwanja wa kutangazwa jamhuri ya nchi hiyo.

Bendera ya Misri