Oct 06, 2021 23:45 UTC
  • Alkhamisi tarehe 7 Oktoba 2021

Leo ni Jumatano tarehe 30 Safar 1443 Hijria sawa na Oktoba 7 mwaka 2021.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1239 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ya sasa ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu zake za kiutawala. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kiroho aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku baada ya siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu. Imam Ridha aliuawa shahidi katika siku kama hii ya leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe".

Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo.

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan.

Sohrab Sepehri

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Bendera ya Ujerumani

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.