Jumatatu tarehe 18 Oktoba 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 18 mwaka 2021.
Miaka 154 iliyopita, ardhi ya Alaska ilidhibitiwa na Marekani. Alaska ni ardhi yenye upana wa karibu kilometa mraba milioni moja na laki tano, huko Amerika ya kaskazini magharibi, ambapo hii leo ni moja ya majimbo ya nchi hiyo. Hadi mwaka 1867 Miladia, Alaska ilikuwa ikidhibitiwa na Russia, hata hivyo katika kipindi hicho mfalme wa wakati huo wa Urusi ya zamani hakutilia maanani umuhimu wa ardhi hiyo na hivyo mwezi Oktoba mwaka 1867 Miladia akaamua kuiuza kwa Marekani. Ni vyema ifahamike kuwa, hii leo Alaska inahesabika kuwa moja ya majimbo tajiri sana ya Marekani ambapo mwaka 1960 kulivumbuliwa mafuta na kuanza kuchimbwa katika eneo hilo hadi leo.

Siku kama ya miaka 150 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allama Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.
Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita alifariki dunia msomi wa Uingereza na mvumbuzi wa mashine ya kikokoteo (Calculator) kwa jina la Charles Babbage. Mwaka 1812 Miladia, Babbage aliasisi taasisi ya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza elimu ya hisabati na akiwa na miaka 24 akateuliwa kujiunga na taasisi ya ufalme ya Uingereza. Ni baada ya hapo ndipo akaanzisha harakati ndefu za utafiti wa kuunda mashine hiyo ya hesabu ambapo hadi kufikia mwaka 1833 Miladia akafanikiwa kuvumbua chombo hicho ambacho kilikuja kuwa mashuhuri kwa jina la Babbage. Baada ya hapo karne moja baadaye wasomi mbalimbali waliifanyia marekebisho muhimu mashine hiyo sanjari na kuifanya itumie nishati ya umeme. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Charles Babbage akatambuliwa kwa jina la baba wa kikokoteo (Calculator).
Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, Redio ya BBC iliasisiwa huko Uingereza. Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini mwaka 1927 redio hiyo iliwekwa chini ya usimamizi wa serikali na ikamilikiwa na serikali ya London. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza. Licha ya kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa propaganda wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, msomi aliyegundua umeme Thomas Edison alifariki dunia. Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa. Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara moja ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.
Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hassan Sadr mmoja wa maulama mahiri wa Kiislamu. Alikuwa mmoja wa mafakihi ambao walipata daraja ya Ij’tihad katika kipindi cha ujana. Sayyid Hassan Sadr alikuwa katika orodha ya walimu mashuhuri katika Chuo KIkuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sadruddin katika elimu ya fikihi, Usul, Itikadi, falsafa na hadithi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Sayyid Hassan Sadr ni Tahsil al-Furu’u al-Diniyyah fi Fikih al-Imamkiyah na Taasis al-Shiyah.