Jumatano, Oktoba 20, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 20 mwaka 2021 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 1153 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Jorjani alifunzwa masomo hayo ya kidini na Qadhi Mkuu wa mji wa Rei ulioko karibu na Tehran ya leo. Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi na miongoni mwake ni "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran.

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya zilifanikiwa kuziangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.
Miaka 69 iliyopita muwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, dikteta wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.