Jumapili, 24 Oktoba, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 24 Oktoba 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1496 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake, Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Alipotimiza umri wa miaka 40, Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja. ***

Siku kama hii ya terehe 17 Rabiul Awwal miaka 1360 iliyopita pia alizaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani. ***

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa. Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.***

Tarehe 24 Oktoba miaka 92 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street. Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake. Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao. ***

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa. Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo. Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani. ***

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo. Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji. ***

Na miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati. Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Kanali ya Suez. Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967 na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti. ***
