May 23, 2016 05:37 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 23

Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyotawala nyuga za michezo kote duniani ndani ya siku saba zilizopita.


Iran yatwaa tena Kombe Ubingwa Mieleka ya Greco-Roman

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara ya tano imetwaa Kombe la Dunia la Mieleka ya Greco-Roman baada ya kuibamiza Russia katika kipute cha fainali ya duru ya 34 ya mashindano hayo. Katika fainali hiyo iliyopigwa Ijumaa katika uwanja wa Shiraz, kusini mwa nchi, vijana wa Iran waliwalemea mahasimu wao wa Russia na kujizolea alama 8-0. Siku hiyo hiyo, timu ya mieleka mtindo wa Greco-Roman ya Iran ililemea Uturuki na kujipatia pointi 7-1. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu amewapongeza wanamieleka hao wa Iran kwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya tano. Russia ambayo iliibuka ya pili ilitwaa medali ya fedha huku mshindi wa tatu ambaye ni Uturuki wakiondoka na medali ya shaba baada ya kuilemea Kazakhstan. Katika mashindano hayo yaliyoanza Alkhamisi na kumalizika Ijumaa, timu zingine zilizoshiriki n pamoja na Ujerumani, Ukraine na Belarus. Timu ya taifa ya mieleka ya Iran ya Kiislamu imewahi kutwaa kombe hilo katika mashindano ya mwaka 2010, 2011, 2012 na 2014.


  Shahrdari ya Tabriz yashinda mashindano ya baiskeli ya Tour de Iran


Timu ya mchezo wa kuendesha baiskel ya Shahdari ya mkoa Tabriz nchini hapa imetwaa ubingwa wa duru ya 31 ya Mashindano ya Kimataifa ya Uendeshaji Baiskeli yaliyofanyika nchini. Katika siku ya mwisho ya mashindano hayo Jumatano, timu hiyo iliibuka kidedea kwa kuendesha baiskeli umbali wa kilomita 1,005 kwa kutumia jumla ya masaa 72, dakika 20 na sekunde 07. Timu hiyo ya Tabriz imefuatiwa kwa karibu na Pishganam ya Yazd, iliyomalizakwa kutumia masaa 72, dakika 35 na sekunde 38 huku UCI ya Kazakhstan ikifunga orodha ya tatu bora, dakika 12 baada ya mshindi wa pili. Mapema siku hiyo, Yevgeniy Gidich wa Kazakhstan aliibuka kidedea katika safu ya mtu moja, kwa kuendesha umbali wa kilomita 114 kwa kutumia masaa 2, dakika 44 na sekunde 14 na kutwaa medaliya dhahabu. Nafasi ya pili nay a tatu katika kitengo hicho kiliwaendea waendesha baiskeli kutoka Japan na China. Duru za 31 ya mashindano ya Tour of Iran (Azarbaijan) ilianza Mei 13 na kufunga pazia lake Mei 18. Jumla ya timu 21 kutoka nchi 16 zikiwemo Armenia, Australia, China, Georgia, Iran, Kazakhstan, Malaysia, Morocco, Uturuki na Uzbekistan zimeshiriki mashindano hayo ya kimataifa, ambayo kwa mara ya kwanza timu ya Marekani imeyashiriki.


Yanga yazidi kung'ara CAF, yatinga robo fainali


Jiji la Dar es Salaam siku ya Ijumaa lilisimama kwa muda, wakati mabingwa wa Tanzania, Yanga walipowasili wakitokea Angola walikofuzu hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup). Mamia ya mashabiki wa Yanga walianza kumiminika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi na hadi kufikia saa nane mchana hali uwanjani hapo ilikuwa si ya kawaida. Pia mashabiki wa Yanga walijipanga barabarani katika maeneo mbalimbali kuanzia Uwanja wa Ndege, Kipawa, Vingunguti na Tazara, ambapo mara kadhaa msafara wa basi la wachezaji wa Yanga uliokuwa ukiongozwa na bodaboda kadhaa ulilazimika kusimama mara kwa mara sababu ya mashabiki walikuwa wanataka kuwaona. Kivutio kikubwa katika mapokezi hayo alikuwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyepangua penalti ya dakika ya 90, ambaye mashabiki walikuwa wakimgombea kutaka kumbeba. LICHA ya juzi kufanikiwa kuing’oa kwa mbinde Sagrada Esperanca ya Angola katika mtoano kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga imeendelea kunung’unikia uchezeshaji wa mwamuzi Hamada el Moussa Nampiandraza na wenzake kutoka Madagascar. Wamesema hawataishia kunung’unika tu, bali watakwenda mbali zaidi ya kulitaka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumsimamisha Nampiandraza. Mwamuzi huyo alisaidiwa na Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina, pia raia wa Madagascar. Katika mchezo huo uliofanyika katika mji wa `mashambani’ wa Dundo ulioko umbali wa kilometa zaidi ya 1,300 kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda, wenyeji walishinda kwa 1-0, lakini matokeo hayo yalikuwa machungu kwa wenyeji, kwani tayari walishaharibu katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam baada ya kukubali kuchapwa 2-0. Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.


 Mau U yatwaa Kombe la FA


Manchester United wameshinda Kombe la FA baada ya kuwalaza Crystal Palace 2-1 katika fainali iliyochezewa uwanja wa Wembley. Ni mara yao ya kwanza kushinda kikombe hicho tangu 2004. Mabao ya Manchester United yalifungwa na Juan Mata na Jesse Lingard. Bao la kufutia machozi la Crystal Palace limefungwa na Jason Puncheon. Ushindi huo ni nafuu sana kwa meneja wa Manchester United Louis van Gaal ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutokana na kutofana kwa klabu hiyo. Kwa ushindi huo, Manchester United wamefikia rekodi ya Arsenal kwa kushinda kombe hilo mara 12. Akizungumza baada ya mechi hiyo, Van Gaal alisema amefurahia sana kushinda kikombe hicho. "Ni muhimu sana kushindia klabu kikombe hiki, kwaa mashabiki, na mimi pia kwa sababu sasa nimeshinda katika mataifa manne, na si mameneja wengi wamefanikiwa kufanya hivyo," amesema.


Sevilla yatwaa Kombe la Uropa


Klabu ya Uhispania ya Sevilla imetwaa Kombe la Ulaya kufuatia ushindi wake dhidi ya Liverpool ya Uingereza, kwa kuwatandika mabao 3-1. Hii ni mara ya tatu mfululizo klabu ya Sevila kutwaa Kombe hili la Ulaya. Liverpool ndio walianza kuliona lango la Sevilla. Hata hivyo klabu hii ya Uingereza ilitawala na kuongoza katika kipindi cha kwanza, lakini Sevilla walisawazisha mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na kufanikiwa kukuingiza mabao mawili ya ushindi. Bao la Liverpool lilifungwa na Daniel Sturridge (1-0) katika dakika ya 35. Bao la kusawazisha la Sevilla lilifungwa na Gameiro (1-1) katika dakika ya 45, Coke alihitimisha kwa bao la pili (1-2) katika dakika ya 64, kabla ya ya kufaulu kutumbukiza wavuni bao la tatu (1-3) katika dakika 70. Wadadisi katika masuala ya soka wanabaini kwamba ushindi huu wa Sevilla utapelekea vilabu vya Uhispani kuongoza katika mashindano makubwa msimu huu. Ushindi huo wa Sevilla unamaanisha kuwa vilabu vya nchi ya Hispania vitatawala katika mashindano makubwa ya soka msimu huu. Fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya itachezwa Mei 28 ambapo Real Madrid itakua inavaana na Atletico Madrid.


Bolt aandikisha rekodi mpya?


Bingwa mara sita wa michezo ya Olimpiki kutokana Jamaica, Usain Bolt ameandikisha muda wake bora zaidi msimu huu baada ya kutimka mbio za mita 100 nchini Jamhuri ya Czech. Bolt alikimbia kwa chini ya sekunde 10 kwa mara ya kwanza, na kumaliza kwa sekunde 9.98 katika mashindano ya Golden Spike mjini Ostrava.Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukimbia Ulaya mwaka huu, na alijikwamua baada ya kuanza vibaya kwa kumshinda Ramon Gittens. Alimaliza mbele ya Gittens kwa sekunde 0.23. Bolt anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za 100m na 200m na kabla ya mbio hizo Ostrava alisema atalenga kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za 200m mjini Rio mwezi Agosti. Bolt alitumia sekunde 10.05 mbio zake pekee alizokimbia msimu huu, katika Cayman Islands Invitational Meet. Mwanariadha huyo wa umri wa miaka 29 alipokea matibabu ya misuli ya paja baada ya mashindano hayo. Alichukua likizo baada ya mashindano ya ubingwa wa riadha duniani jijini Beijing Agosti mwaka jana ambapo alishinda dhahabu katika mbio za 100m, 200m na 4x100m kupokezana vijiti.


……………………………..…..TAMATI……………………………..


Tags