Oct 27, 2021 00:32 UTC
  • Jumatano tarehe 27 Oktoba 2021

Leo ni Jumatano tarehe 20 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 27 mwaka 2021.

Miaka 993 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu aliandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawabun fi Sama'a" na "al Ghinaa wa Al Taaliqatil Kubra fil Furu'u".

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa zaidi ya karne 4. 

Bendera ya Norway

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, ilitwaa rasmi ardhi ya Korea na kuiunganisha na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. 

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu. Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuachia madaraka. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo. Miaka 7 baadaye Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika mwaka 1965. Hata hivyo alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa Jenerali Yahya Khan  aliyekuwa mkwewe. 

Jenerali Muhammad Ayub Khan

Na siku kama ya leo miaka 48 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani, alimu mkubwa na mtaalamu wa elimu ya fiqhi. Ayatullah Zanjani alizaliwa mwaka 1308 Hijiria na kupata elimu ya awali na ya juu huko Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya hapo alielekea Qum kwa ajili ya kuendelea na elimu ambapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama Abdul-Karim Haeri Yazdi na Muhammad Hujjat Kuh-Kamarei. Baada ya Ayatullah Muhammad Hujjat kufariki dunia, Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani alichukua wadhifa wa kuongoza Swala ya jamaa katika shule ya Faidhiyya. Katika muongo wa 1320 Hijiria Shamsia, msomi huyo alikutana na Imam Ruhullah Khomeini (MA) na kushirikiana naye katika vikao vingi vya kielimu. Msomi huyo ameandika vitabu zaidi ya ishirini vikiwemo vya 'Arbaiin' 'Afwahur-Rijaal' na 'Furuqul-Ahkaam'.

Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani,