Oct 28, 2021 22:58 UTC
  • Ijumaa tarehe 29 Oktoba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 22 Mfunguo Sita 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Oktoba mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (SAW). Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao. 

Mabaki ya ngome ya Mayahudi wa Bani Nadhir

Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake.

Kemal Ataturk

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa. Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza. Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah.

Ayatullah Sayyid Hassan Modarres

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Na siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanawaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim.