Jumatano, Novemba 3, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 3 Novemba 2021 Milaadia.
Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1080 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man karibu na mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Idlib. Alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."
Miaka 65 iliyopita muwafaka na siku hii ya leo, wakati wa kujiri mashambulio ya askari wa utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Misri, wanajeshi wa utawala huo waliuvamia mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo. Baada ya kuukalia kwa mabavu mji huo, askari hao waliwanyonga askari 25 wa Kimisri. Unyama wa askari hao haukuishia hapo, kwani waliishambulia hospitali ya mkoa mjini Khan Yunis na kuwaua kwa umati wauguzi, madaktari na wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Watu wapatao 275 waliuawa katika mashambulio hayo.
Siku kama ya leo Miaka 53 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.
Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Jenerali Jean-Bedel Bokassa mtawala wa Afrika ya Kati. Bokassa alichukua madaraka mwaka 1921 kupitia mapinduzi ya kijeshi, baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais David Dacko kwa uungaji mkono wa Ufaransa. Katika miaka 14 ya utawala wake, kiongozi huyo alitenda jinai na mauaji mbalimbali na kujilimbikizia mali nyingi.