May 23, 2016 09:44 UTC
  • Familia Salama-2 (lishe)

Moja kati ya nukta muhimu za afya ya mwanadamu ni lishe bora. Lishe kimsingi ni sayansi inayobainisha kuhusu virutubishi na viungo vingine katika chakula na uhusiano wake katika ustawi wa mwili, afya, maradhi n.k. Chakula tunachokula ndicho kinachoupatia mwili virutubisho . Ili mwili upate virutubisho hivyo kutoka kwenye chakula tunachokula, chakula hicho lazima kivunjwevunjwe kwanza. Zoezi hilo huanza kwa kutafunwa chakula mdomoni, kumezwa na kisha kufika tumboni.

Kikifika tumboni, chakula hicho huchanganyika na maji na vimimina vingine zikiwemo tindikali na kisha kuelekea kwenye utumbo mdogo. Virutubisho hufyonzwa na kuingia kwenye mfumo wa damu kupitia kuta za utumbo mdogo na kusambazwa mwilini. Mabaki yasiyofaa mwilini huelekea kwenye utumbo mkubwa na kisha kutoka nje ya mwili. Virutubisho hivyo ambavyo huchukuliwa na mwili vinaweza vikagawanywa katika makundi sita makuu: Protini (proteins), wanga (carbohydrates), mafuta (fats), vitamini (vitamins), madini (minerals) na maji. Lishe ni muhimu katika dunia ya leo kutokana na ongezeko la matatizo yanayotokana na lishe duni au lishe isiyo sahihi. 

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa asilimia 45 ya watu walio na umri wa kati ya miaka 15-64 duniani wanakumbwa na tatizo la unene.

Aidha, kwa masikitiko, uchunguzi umebaini kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la watoto wenye tatizo la unene kote duniani.

Takwimu zinaonesha kuwa waliowengi duniani wanaishi katika nchi ambazo unene wa kupindukia huua watu wengi zaidi kuliko ukosefu wa chakula. Mbali na unene, utumiaji wa vyakula vilivyo na mafuta na sukari kupita kiasi, utumiaji wa chakula kilichotengenezwa viwandani na unywaji soda na pombe, yote hayo huchangia katika kudhoofisha kinga ya milii, kusababisha maradhi na hatimaye kifo.

Piramidi ya Chakula Bora ni muongozo sahali wa kuhakikisha kuwa mwanadamu anapata lishe bora na sahihi. Kila mwanadamu anapaswa kuwa na mpango maalumu wa anuai ya chakula chenye kiwango cha kutosha cha carbohydrate, mafuta, protini, vitamini, madini, maji na fiber au ufumwele.

Vyakula hivyo ni muhimu katika ustawi na utendaji kazi sahihi mwilini pasina kuwepo na madhara. Iwapo nukta hizo za lishe zitazingatiwa katika kila mlo basi tunaweza kusema mpango wa chakula kila siku una mlingano mzuri.

Afya inatokana na lishe nzuri na ishara za afya ni kuwepo uwiano wa uzito na urefu (BMI) na kipimo hicho huenda sambamba na umri. Aidha nukta zingine zenye kuashiria afya bora ni kama vile ngozi inayongara, kucha salama zenye rangi takribani ya waridi. Halikadhalika mwenye afya nzuri anapaswa kutembea wima na kupiga hatua imara, na macho kuweza kutazama huku na kule na kuona vizuri. Halikdhalika wataalamu wanasema ishara nyingine ya mtu mwenye afya ni kuwa na hamu nzuri ya chakula, kuenda choo bila matatizo na uwezo mzuri wa kutafakari. Lakini pamoja na hayo inafaa kukumbusha hapa kuwa kutumia kupita kiasi baadhi ya vyakula kama vile nyama nyekundu huwa na madhara kwa afya na yamkini hata kukasababisha saratani. Aidha kutumia kiasi kidogo cha vyakula aina ya nafaka yenye vitamin D hupelekea kuibuka maradhi ya kiakili kama vile tabia ya uchokozi.

Idadi kubwa ya watu hudhani kuwa baadhi ya maradhi kama vile shinikizo la damu, unene, maradhi ya moyo n.k ni maradhi ya kurithi kutoka kwa wazazi. Ingawa kuna umuhimu katika kuzingatia historia ya familia katika maradhi kama hayo tuliyoyataja, lakini kwa mtazamo wa wataalamu wa lishe, aina ya lishe huchangia katika kuandaa mazingira ya mtu kurithi aina fulani ya ugonjwa ambapo huupata ugonjwa huo mapema au baadaye katika umri wake. Uchunguzi umeonyesha kuwa, unene, ugonjwa wa kisukari, mshutuko wa moyo, ongezeko la shinikizo la damu, mshtuko wa ubongo, maradhi ya mifupa, anui za saratani n.k ni maradhi ambayo yanaweza kuzuiwa kwa lishe bora na sahihi.

Kwa hivyo kwa kutambua ufahamu wa lishe bora, na kutumia makundi yote ya vyakula sambamba na kupunguza utumizi wa chumvi na mafuta aina ya trans fatty acids ni nukta muhimu katika kuboresha afya ya mwili na kuzuia maradhi hatari. Kwa kufafanua kuhusu trans fatty acids tunaweza kusema kuwa neno acid kwa kiswahili maana yake ni tindikali na neno fat maana yake ni mafuta, na hususan yale yasiyoyeyuka au kumininika kwa urahisi. Mafuta yasiyomiminika ni yale ambayo asili yake ni katika hali ya kuganda yanapokuwa katika mazingira ya joto la kawaida kivulini. Hata hivyo neno ’fat’ katika sehemu za makala hii limetumika kwa maana ya mafuta bila kujali kuwa ni yale yanayoganda katika joto la kawaida au ni yale yanayomiminika. Kwa tafsiri hii Fatty acids zinaweza kuitwa kwa kiswahili kuwa ni Tindikali za mafuta. Kwa muda mrefu sasa, wataalamu wa afya na lishe, wanashauri watu kuhusu athari za ulaji wa kiasi kikubwa cha aina zote za mafuta.

Ulaji wa mafuta hasa yale yanayotokana na wanyama, yanahusishwa na matatizo mengi ya kiafya kama vile magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa ya mishipa ya damu n.k. Kutokana na sababu hiyo, ulaji wa mafuta mengi umekuwa ukihusishwa na kutokea kwa vifo vya watu wengi duniani.

Hali kadhalika ili kuzuia magonjwa na kuwa na lishe bora kuna haja ya kupunguza utumizi wa aina mbali mbali za sukari na badala yake kutumia mboga , matunda, maharage, nafaka kamili (whole grains), mkate wa ngano ambayo haijakobolewa sana (whole wheat). Lishe hiyo bora inapaswa kuendamana na mazoezi ya kila siku. Kwa msingi huo lishe bora na sahihi pamoja na mazoezi huimarisha uwezo wa kimwili na kumpa mwanadamu afya bora wakati wa uzeeni na hata kupunguza au kuzuia baadhi ya magonjwa na hilo likifanyika huwa ni kwa maslahi ya uchumi wa kila familia na jamii.


Tags