Dec 13, 2016 09:38 UTC
  • Familia Salama (20)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huangazia masuala yanayohusiana na familia.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia suala la uchumi wa familia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Kama tunavyojua, familia ni kituo kidogo zaidi katika jamii. Familia ni sehemu asili ya maisha, matumizi, malezi na elimu ya mwanadamu. Tabia na mienendo ya watu wengi hutegemea  utamaduni waliolelewa nao katika familia. Kwa msingi huo, familia ni kigezo. Hivyo, iwapo familia zitakuwa kigezo bora cha maadili na sambamba na hilo zikaweza kuwa na misingi bora ya kiuchumi, jamii nayo itaweza kustawi ipasavyo. Jamii kama hiyo itakuwa na watu wenye maadili mema, nidhamu na walio na utamaduni mzuri wa kazi na uzalishaji. Ni kwa sababu hii ndio katika jamii zote, ziwe ni zile ambazo zinaanza kustawi, zinazostawi na zilizostawi, familia ni msingi muhimu wa uzalishaji na usambazaji  bidhaa na huduma katika jamii. Moja ya nukta muhimu katika jamii kama hiyo ni kuweza kutayarisha kizazi cha wafanyakazi na hivyo kuhakikisha kizazi kinaendelea kuwepo. Ni kwa msingi huu ndio wataalamu wa uchumi wakasema kuwa, familia ni msingi muhimu wa uchumi wa jamii zote.

Lakini kabla hatujazungumza kuhusu "uchumi wa familia" tunapaswa kufahamu kwa kifupi kuhusu maana ya neno "uchumi: na kisha baada ya hapo tubainishe uhusiano wa uchumi na familia. Katika kubainisha maana ya neno uchumi, kwa kawaida hutajwa maneneo mawili , nayo ni 'uhaba" na "mahitajio au matakwa ya mwanadamu". Hii ina maana kuwa, bidhaa na huduma huwepo kwa lengo la kuhudumia matakwa ya mwanadamu. Iwapo kutakosekana huduma na bidhaa basi maisha ya mwanadamu yatakumbwa na matatizo makubwa. Idadi kubwa ya bidhaa zinazozalishwa hutokana na mali ghafi iliyo katika ardhi. Bidhaa nyinginezo kama vile magari, ndege n.k hutokana na uwezo wa mwanadamu kudhibiti maliasili katika ardhi na kuzitumia kwa manufaa yake na hilo ndilo hutajwa kuwa ni ''rasilimali'. Kwa msingi huo mwanadamu au 'nguvu kazi' ni hitajio muhimu katika kuzalisha bidhaa na huduma. Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa mahitajio muhimu katika uzalishaji bidhaa na huduma ni, ardhi, mali asili, nguvu kazi na uwekezaji.

"Rasilimali" ni natija ya jitihada za mwanadamu kudhibiti maliasili na ardhi. Kadiri mali asili za nchi zinapokuwepo kwa wingi na kadiri uwezo wa kifikra wa mwanadamu unapokuwa mwingi, na kadiri uwekezaji wa lazima pamoja na suhula zinapokuwepo  katika jamii, basi  kiwango cha uzalishaji wa bidhaa na huduma  huimarika. Lakini kuna uhaba au uchache wa nukta hizo katika jamii nyingi. Katika upande wa pili, mahitajio ya mwanadamu hayana mipaka na kadiri kunavyoshuhudiwa ustawi wa elimu na sayansi mahitaji haya huongezeka.

Sayansi ya uchumi inatufunza namna ya kutumia vyanzo vichache kupata faida au mafanikio makubwa. Familia pia ina nukta hizo mbili za uzalishaji yaani, 'rasilimali' pamoja na 'nguvu kazi'. Kwa hivyo familia ni kituo cha kiuchumi na uchumi wa familia unaweza kutajwa kuwa ni usimamizi na utumizi bora wa vyanzo vya utajiri katika familia.

 

Hapa tunapaswa kuuliza je, hivi vyanzo vya utajiri ni nini hasa? Tunaweza kuweka ordhoha kamilia ya vyanzo hivyo kuwa ni fedha, mahala inapoishi familia na shuhula zilizopo. Utajiri huu unatafuatiana kutoka familia moja hadi nyingine lakini kuna sifa moja ya pamoja nayo ni 'uhaba'. Bila shaka umewahi kusikia watu wengi wakisema: "Laiti nigelikuwa na wakati au fursa zaidi, laiti ningelikuwa na nyumba kubwa zaidi, laiti ningelikuwa na pesa nyingi zaidi, na laiti nyingine nyingi. Hata wale ambao wana vyanzo vya kutosha vya fedha pia hutamani kupata zaidi ya walivyo navyo.

Kila familia hupenda kula chakula bora zaidi, kuvaa nguo  maridadi zaidi na kuishi katika nyumba bora zaidi sambamba na kuenda safari za starehe mara kwa mara.

Lakini kile kilicho wazi ni kuwa, familia zina vyanzo vya fedha vyenye mipaka na kwa msingi huo katika aghalabu ya familia, kuwepo na uhaba ni jambo la kawaida.

Hivyo, kila familia, kwa kutegemea vyanzo vyake vya fedha, hulazimika kuchagua miongoni mwa matakwa ya wanafamilia na kuchukua maamuzi ambayo yatapalekea wanafamilia wote waweze kuridhika. Ni kwa msingio huo ndio familia huchagua kinachotakiwa na kinachoweza kufikiwa. Yaani huamua ni kitu gani kitumike, kiasi kitakachotumika na namna kitakavyotumiwa, ni nani afanye kazi, masaa mangapi afanye kazi, ni vipi pato la kazi hiyo litumike, n.k. Haya ni maswali ambayo hujitokeza kila siku katika familia. Maamuzi ya kiuchumi katika familia yanahitaji chaguo sahihi na hivyo chaguo ni roho ya uchumi wa familia.

Wapenzi wasikilizaji makala yetu inafikia tamati hapa kwa leo. Jiungeni nasi katika makala yetu ijayo tuendelee kujadili mada hii.

 

Tags