Dec 13, 2016 09:42 UTC
  • Familia Salama (21)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaendelea kujadili suala la uchumi wa familia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Wakati  tunapozungumza kuhusu uchumi wa familia tunapaswa kufahamu kuwa uchumi huu hauhusu familia za matajiri pekee kwani suala hili ni la familia zote hata zenye pato la chini hasa kwa kuzingatia kuwa katika familia kama hizo hukosekana mlingano baina ya pato na matumizi.

Kile ambacho kinapaswa kufahamika katika uchumi wa familia ni kuwa, ongezeko la pato halimaanishi kuboreka hali ya maisha kwani aghalabu ya ongezeko la pato huambatana na ongezeko la gharama za kimaisha.

Kwa msingi huo iwapo gharama zitongezeka hilo linamaanisha kuwa kunahitajika usimamizi bora wa kifedha ili familia iweze kuendelea na maisha ya kila siku pasina kuwepo matatizo.

 

Uchumi wa familia kwa kiasi kikubwa huwa na uhusiano wa karibu na kazi zinazofanywa na wanafamilia. Kwa msingi huo kunapaswa kuwepo utaratibu na mpango maalumu wa kufuatilia kazi zinazofanywa na wanafamilia ambao aghalabu huwa ni wazazi wawili. Ili familia iweze kufanikiwa, kila mwanafamilia anapaswa kutekeleza maamuzi yanayochukuliwa katika familia kuhusu utumizi wa fedha ili wote waweze kufanikiwa.

Katika hali ya kawaida,  usimamizi wa kiuchumi katika familia hutegemea kiwango cha pato la wanafamilia wanaofanya kazi. Kama ambavyo  wazazi wana jukumu la kusimamia masuala ya kiroho na kijamii katika familia, hali kadhalika pia wana jukumu la kusimamia kikamilifu suala la gharama  na kuleta mlingano baina ya pato na matumizi katika familia.

Katika maisha ya kila siku katika familia, kuna maamuzi muhimu ambayo huchukuliwa. Katika kila familia kuna bajeti ya bidhaa za kutumika kwa muda mrefu kama vile televisheni, friji, fanicha, gari, na hata kununua nyumba. Kisha kuna bajeti ya kunaunua bidhaa za kutumiwa na kumalizika haraka kama vyakula n.k na baada ya hapo kuna bajeti ya masuala ya kistarehe. Kwa kutegemea idadi ya watoto, familia inapaswa kuchukua maamuzi sahihi kuhusu kiwango cha elimu na afya kwa wanafamilia. Kwa mfano kunapaswa kuchukuliwa maamuzi sahihi ni shule ipi mtoto asome na hilo litegemee pato la familia. Aidha katika kupata huduma za afya kila familia inapaswa kuzingatia pato lake ili kuepuka kurundikana gharama ambazo itakuwa vigumu kuzimudu.

Moja ya njia za kupunguza gharama za matumizi ya kila siku katika familia ni kulinganisha bei ya bidhaa mbali mbali kabla ya kununua. Kuchunguza au kufanya utafiti kabla ya kununua hupelekea kununuliwa bidhaa au huduma bora na kwa bei nafuu ambayo familia inaweza kumudu. Kwa mfano katika kununua bidhaa za matumizi kama vile televisheni au simu za mkononi, kuna haja ya kunuanua bidhaa yenye kiwango kizuri ili isiharibike haraka na wakati huo huo kuhakikisha bei ya bidhaa haitailetea familia mzigo mkubwa.

 

Nukta nyingine muhimu katika uchumi wa familia ni wakati, zama au fursa. Nukta hii ina umuhimu wa kipekee ikilinganishwa na mengine yote kwa sababu wakati au fursa haipo wakati wote. Wakati ukishapita umepita na hauwezi kurudi tena. Fursa nayo ni vivyo hivyo, ikijitokeza inapaswa kutumiwa la sivyo yamkini haitapatikana tena. Mwanadamu anawajibika kuhusu kile alichonacho na wakati pia ni kati ya mambo ambayo mwanadamu anapaswa kuyatumia ipasavyo. Kwa msingi huo, wakati, zama au fursa ni mambo yenye umuhumu mkubwa kwa kila familia na hivyo kila familia inapaswa kuwa na mpango maalumu wa kutumia wakati na fursa zilizopo ili kujiimarisha kiuchumi.

Familia isiyo na mpango na ratiba maalumu ni kama shirika ambalo halina muelekeo wala malengo. Ni wazi kuwa malengo ya wenye kuunda familia hayawezi kufikiwa iwapo mkuu au kiongozi wa familia hatakuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha kuhusu vyanzo alivyo navyo. Katika kujenga uchumi imara wa familia awali kuna haja ya kufahamu malengo ya familia husika. Kwa msingi huo mipango jumla ya familia itaainishwa  kisha mipango midogo itatekelezwa huku lengo kuu likiwa ni kutekeleza mipango asili ya familia. Mipango hiyo inaweza kuwa katika daraja tatu za upeo wa zama na wakati yaani malengo ya muda mrefu, malengo ya muda wa kati na malengo ya muda mfupi. Familia inaweza kutekeleza malengo ya muda mrefu kwa kuzingatia vyanzo vya fedha kama vile milki au utajiri na pato pamoja na wakati uliopo wa kufikia lengo hilo.

Ni wazi kuwa malengo kama vile ya kuwasomesha watoto kwenye vyuo vikuu hayawezi kufikiwa siku moja na yanahitajia maandalizi maalumu.

Kwa hivyo kwa kuwepo mpango wa muda mrefu, familia inaweza kutekeleza mpango wa muda mfupi na muda wa kati. Mipango yote hiyo ya daraja tatu inapaswa kuwa na uhusiano na mlingano ili isivurugike.

Kwa mfano katika kuwasomesha watoto kwenye vyuo vikuu, familia inapaswa kuwa na mpango wa kuwaandalia watoto mazingira mazuri ya kuwawezesha kufika chuo kikuu na hili linawezekana kupitia kuwapeleka katika shule nzuri katika mpango wa kati.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanaamini kuwa,  familia ikiwa na mipango maalumu na uwezo wa kufikia malengo hayo, basi maisha yatakuwa mazuri na yenye maelewano. Aidha ili kufikia malengo hayo, wataalamu wanasema wanafamilia wanapaswa kuacha ubinafsi, wawe wakweli na wenye kushirikiana.

 

 

Tags