Dec 13, 2016 10:13 UTC
  • Familia Salama (22)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo ambayo ni ya mwisho,  tutaendelea kuangazia suala la uchumi wa familia kwa kuchunguza ni vipi familia ikabiliane na hali ngumu ya kiuchumi.  Wakati wa hali mbaya ya kiuchumi, aghalabu ya familia hukumbwa na matatizo ya kifedha na kiuchumi.

Matatizo haya huwa ni ya aina mbali mbali na hata kupelekea baadhi ya familia kupoteza akiba ya uzeeni.  Katika hali mbaya ya kiuchumi baadhi ya wazazi hupoteza kazi  huku baadhi ya familia zikishindwa kujimudu katika kukidhi mahitajio ya kila siku na hivyo kulazimika kuchukua mikopo. Ukopaji wakati mwingi huwa na athari mbaya za kiuchumi na kijamii katika familia

Lakini pamoja na hayo wataalamu wa uchumi wanapendekza njia mbali mbali za kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa fedha katika familia ili kuzuia wanafamilia kuathirika vibaya.

Moja ya njia muafaka  za kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi katika familia ni kupunguza gharama zisizo za dharura. Katika kila familia kunapaswa kuwa na bajeti ya kila kitu ili kwa njia hiyo kupunguza gharama ambazo hupelekea kuwepo nakisi ya bajeti. Kwa msingi huo nidhamu ya kifedha katika familia ni jambo la dharura. Iwapo familia itafanikiwa kupata pato lisilotarajiwa, fedha hizo zinapaswa kuwekwa akiba badala ya kuzitumia kwa starehe au kujiingiza katika ununuzi wa bidhaa zisizo za dharura. Wakati wa kupanga bajeti ya familia inashauriwa kuwa, daima kuwepo na mpango wa kuweka akiba na fedha hizo zinaweza kupatikana kwa kupunguza matumizi yasiyo ya dharura. Njia bora ya kuweka akiba ni kufungua akaunti maalumu katika benki kwa ajili ya kuweka fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya dharura.

Bila shaka si jambo rahisi kuweka akiba kwani kuna vishawisi vingi sana vya kutumia pesa lakini ni muhimu kukumbuka kuwa fedha za akiba huweza kuiokoa familia wakati inapokumbwa na msukosuko wa kifedha. Ni vizuri kuwa na mpango wa matumizi ya kistarehe katika familia kama vile ununuzi wa zawadi, sherehe za kuzaliwa, safari n.k lakini iwapo una wasi wasi kuwa gharama hizo zitaibua matatizo basi ni vyema kuachana nazo na kuweka fedha hizo katika akiba. Katika kupanga bajeti ya familia kuna ulazima wa kutenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kulipia huduma za kila siku kama vile za umeme, maji, n.k na pia kuwepo fedha za kuwapa wanafamilia kwa mfano nauli ya watoto wanapokwenda shule au fedha za kutumia kununua chakula wakiwa shuleni n.k. Katika kuwapa watoto pesa za matumizi haipaswi kuwapa pesa nyingi ghafla bali ni muhimu kuwapa kiasi kidogo cha pesa na kufuatilia matumizi yake na kisha kadiri umri unavyosonga mbele kiasi hicho kiongezwe lakini kwa usimamizi wa karibu kuhusu matumizi.

Aidha kunapaswa kutengwa kiasi fulani cha pesa nyumbani daima kwa ajili ya matumizi ya dharura yanayoweza kujitokeza.

Kama tulivyotangulia kusema, kuweka akiba ni njia ya hakika ya kujizuia kukumbwa na matatizo ya kifedha katika siku za usoni.  Aidha akiba hiyo inaweza kutuzamwa kama mradi ambao unaweza kutumiwa katika biashara au kununua ardhi, nyumba au hata gari. Hali kadhalika akiba ya fedha inaweza kutumiwa kuwasomeshea watoto au kuwaozesha. Moja ya njia muafaka za kuhakikisha kuwa fedha za akiba hazitumiki kusikotakikana ni kuwa na akaunti maalumu katika benki na kujiwekea sharti kuwa fedha hizo zisitumike isipokuwa tu katika dharura isiyoweza kuepukika.

 

Pia kuwa na bima ya maisha katika zama hizi ni jambo muhimu na linaloweza kutengewa bajeti katika uchumi wa familia. Bima ya umri huzuia familia kukumbwa na matatizo na msukosuko wakati mwanafamilia anapoaga dunia.

Hakuna mtu yeyote anayejua ni lini atakapofariki wala anayetaka familia yake ikumbwe na matatizo wakati atakapofariki. Ingawa Bima ya umri haina faida kwa mwenye kuiweka lakini ni hakikisho la kuilinda familia. Aghalabu ya bima za umri huwapa wanafamilia kiasi  cha fedha kwa wanaondokewa na mpendwa wao na hivyo kuepusha msukosuko wa kifedha katika familia. Katika baadhi ya nchi pia kuna bima ya kuachishwa kazi ambapo wakati mtu anapoachishwa kazi kwa sababu yeyote ile huweza kupokea fedha za kumuwezesha kujimudu kimaisha.

Wapenzi wasikilizaji kwa hayo, tunafikia mwisho wa mfululizo wetu huu wa vipindi kuhusu familia salama. Ni matumaini yetu kuwa vipindi hivi vimeweza kuwa na mchango mzuri katika kuimarisha afya ya familia. Tunawatakia nyote maisha mema yaliyojaa fanaka za dunia na akhera.

 

Tags