Alkhamisi tarehe 4 Novemba 2021
Leo ni tarehe 28 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Novemba 4 mwaka 2021.
Miaka 103 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufalme wa Austria-Hungary ulisalimu amri kwa vikosi vya majeshi ya Waitifaki wiki moja tu kabla ya kufikia tamati Vita vya Kwanza vya Dunia. Utawala huo ambao ndio uliokuwa umeanzisha vita, ulikuwa ukihesabiwa kuwa muitifaki muhimu wa Ujerumani. Hata hivyo kutokana na kushindwa mara nyingi katika vita, ulikubaliana na masharti ya kuacha vita. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Austria-Hungary uligawanywa kwa nchi kadhaa na ukoo wa Habsburg uliokuwa ukitawala ukasambaratika.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Miaka 43 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi."

Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliuawa na Mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada. Rabin alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kuanzia mwaka 1974 hadi 1977 kwa tiketi ya Chama cha Leba. Hata hivyo aliuzuliwa wadhifa huo kwa tuhuma za ubadhirifu. Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.
Rabin aliongoza operesheni kadhaa za mauaji ya kigaidi dhidi ya Waarabu na Wapalestina na kutenda jinai nyingi za kutisha.