May 23, 2016 09:49 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (41)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chtu cha juma lililopita kilijadili na kuzungumzia sifa na tabia mbaya ya kupeleleza na kupekua aibu za watu na kunukuu baadhi ya hadithi zinazohusiana na maudhui hiyo. Mkabala na sifa ya kupeleleza na kuchunguza aibu za watu kuna sifa inayojulikana kama kuficha aibu za watu.

Tabia hii ni miongoni mwa sifa kubwa kabisa za waumini ambazo zimeusia mno katika dini tukufu ya Kiislamu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 41 ya mfululizo huu kitajidi maudhui hii na kukunulieni baadhi ya hadithi katika uwanja huo. Kuweni name hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio kile nilichokuandaline kwa wiki hii. 

*********

Moja ya mambo ambayo yameusiwa na kutiliwa mkazo na dini Tukufu ya Kiislamu ni kuficha na kusitiri aibu za waja wa Mwenyezi Mungu. Kusitiri aibu kinyume na kupeleleza na kufichua aibu za watu ambayalo hupelekea kuibuka ugomvi, mivutano na utengano, lenyewe huwa chimbuko la kuimarika urafiki, huba na kuongezeka hali ya kuaminiana baina ya watu. Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema kuwa: Funika na kustiri aibu za watu kadiri inavyowezekana kama unavyopenda Mwenyezi Mungu afunike na kustiri aibu zako mbele ya macho ya watu.

Mtume Muhammad SAW ambaye ni mwanadamu mkamilifu kabisa na mbora wa viumbe alijipamba na suala la kufunika na kutofichua aibu za wengine na alikuwa akiwausia wafuasi wake kwa kuwaambia: Kila ambaye ataficha na kufunika aibu ya ndugfu yake Mwislamu na kutomuumbua, basi Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama atazistiri aibu zake.

Nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni hii kwamba, makusudio ya kufunika na kutotaja aibu za mtu ni kutofichua mapungufu aliyonayo mtu huyo. Pamoja na hayo jukumu la kuamrishana mema na kukatazana mabaya linalazimu mtu kumueleza ndugu yake Mwislamu aibu na mapungufu aliyonayo, lakini hilo kama tulivyoashiria katika kipindi chetu cha juma lililopita ni jambo ambalo linapaswa kufanyika kwa siri na njia bora na yenye maneno mazuri na ya kuvutia kiasi cha kutomfanya mlengwa achukie.

Viongozi wakubwa wa uislamu wametoa nasaha zenye thamani kubwa mno kuhusiana na kufunika aibu za watu hususan viongozi kustiri aibu za raia. Tunasona katika sehemu ya barua ya Imam Ali bin Abi Twalib AS kwa Malik al-Ashtar kwamba:

"Baina ya watu kuna aibu na mapungufu yaliyojificha, hivyo usiondoe pazia lake. Mwenyezi Mungu mwenyewe anahukumu kuhusiana na mambo ya siri. Ficha na usitiri aibu na mapungufu kadiri unavyoweza ili Mwenyezi Mungu naye asitiri na kuficha aibu zako ambazo unapenda zibakie kuwa ni siri.”

Katika sehgemu nyingine ya nasaha zake kwa viongozi, Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema:

“Wasiwahesabia raia mambo madogo madogo bali fumbia macho mambo mabaya na ongeza kiwango cha thamani yako.”

Moja ya sifa mbaya za kimaadili na kiakhlaqi ni mtu kutoona aibu zake na badala yake kuzingatia aibu za wengine. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa Imam Ali bin Abi Twalib AS ni kuwa;

Aibu na mapungufu makubwa zaidi ni kushughulisdhwa na aibu za wengine ilihali aibu hizo hizo na wewe unazo.

Wanadamu wakubwa na wacha Mungu badala ya kutafuta na kuchunguza aibu za wengine hujichunguza wao wao na kuangalia aibu na mapungufu waliyonayo na kufanya hima ya kujirekebisha.

Imam Ali AS amenukuliwa akisema kuwa, hongera zimuendee mtu ambaye anazingatia aibu zake na anajizuia kufuatilia na kuchunguza aibu za wengine. Tukirejea mafunduisho nay a Uislamu na hadithi tunapata kuwea imesisitizwa na kutiliwa mkazo mtu juu ya suala la mtu kuangalia aibu na mapungufu yake kabla ya kuangalia aibu za wengine. Imam Ali AS anasema: Mtu anayetazama aibu za watu anapaswa kuanza na aibu zake.

Aidha Mtume SAW amaenukuliwa katika hadithi mashuhuri akisema kuwa, ukitaka kutaja aibu za mwanzako kwanza kumbuka aibu zako.

Ukweli wa mambo ni kuwa kuna watu katika jamii ni mahodari mno wa kukosoa watu wengine na kuona aibu na mapungufu ya wenzao lakini mapungufu na aibu hizo hizo na wao wanazo. Hivyo basi mtu huyu kabla ya kutaja aibu za wengine anapaswa kukumbuka kwanza aibu zake.

Kusitiri aibu ni moja ya sifa za Mwenyezi Mungu yaani “Sattar al-Uyuub” mwenye kusitiri aibu.

Mtu ambaye anasitiri aibu za watu hugeuka na kuwa kioo cha Mwenyezi Mungu.

Imekuja katika hadithi kwamba, itakafika Siku ya Kiyama, siku hiyo Bwana Mtume SAW atamuomba Mwenyezi Mungu kwamba, wakati wa kuhesabu amali za watu, umati wake usihesabiwa amali zao mbele ya Malaika, Mitume na umma nyingine. Mtume SAW anamuomba Mwenyezi Mungu umma wake uhesabiw amali na matendo yake kwa namna ambayo mbali na Mtume na Mwenyezi Mungu watu wengine wasifahamu aibu na madhambi ya umma wake. Baada ya Mtume SAW kutoa ombi lake hilo Mwenyezi Mungu atamjibu kwa kusema:

Ewe kipenzi change, mimi ni mwenye huruma zaidi na waja wangu, kwani kama ambavyo wewe hupendi aibu zao zifahamike na watu wengine, mimi pia sipeni na sioni vizuri aibu zao zifahamike hata kwako wewe. Ni kwa sababu hiyo mimi nitalishughulikia mwenyewe suala la kuhesabu amali za zao kiasi kwamba, ili ghairi yangu asipatikane mtu ambaye atafahamu aibu na makosa yao.”

Katika dua nyingi suala la kusitiriwa aibu limezingatiwa mno. Kwa mfano tunasoma katika sehemu ya dua ya 16 ya Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS katika kitabu chenye thamani kubwa cha Sahifat al-Sajjadiyah kwamba:

Ewe Mola wangu ninayekuabudu! Sifa njema na shukurani ni zako, aibu ngapi umenisitiri hukunifedhehi dhambi, ngapi umezifunika kwa ajili yangu hukunifanya niwe mashuhuri kwazo. Makosa mangapi nimeyatenda wala hukunichania pazia la sitara, wala haukunibandika utepe wa chuki ya fedheha yake, wala haukudhihirisha aibu yake kwa atafutaye aibu zangu miongoni mwa majirani zangu na wenye husda ya neema zako kwangu.”

Aidha imekuja katika dua ya Jawshan Kabir: Ewe mwenye kudhihiri uzuri na mwenye kusitiri ubaya.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo.