Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (32)
Assalaam alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote mlipo.
Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni watajika wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na kazi na athari zao. Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari maisha ya alimu na msomi mwingine wa Kishia aliyeishi katika karne ya 11 Hijria ambaye ni Muhammad bin Hussein bin Abdul Swamad Harithi, mashuhuri zaidi kwa majina ya Bahau Din au Sheikh Bahai. Sheikh Bahai alizaliwa mwaka 953 Hijria katika mji wa Baalbek huko Lebanon. Tulibainisha pia kwamba, Sheikh Bahai mbali na kubobea katika elimu na maarifa ya Kiislamu alikuwa hodari pia na mwalimu katika taaluma rasmi na elimu mashuhuri katika zake kama vile hisabati, usanifu majengo, uhandisi, jiografia na nujumu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 32 ya mfululizo huu kitamzungumzia msomi na mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Kishia ambaye si mwingine bali ni Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad mwanafalsafa mkubwa wa Kishia. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.
Historia ya madhehebu ya Ahlul-Baiti (a.s) na maisha ya Maulamaa wa Kishia katika kipindi cha ghaiba ya Maasumu wa mwisho yaani Imam Mahdi (atfs) imekumbwa na hali ya panda shuka. Lakini pamoja na hayo, katika kipindi chote hiki, maktaba ya kifikra ya Ushia imeweza kukabiliana na mifumo mbalimbali ya kifikra na hivyo kuweza kulinda asili yake na kuifanya ibaki hai kama maktaba inayojitegemea. Uwezo huu kwa maktaba ambayo kwa karne nyingi imekuwa ikiandamwa kwa njama mbalimbali na watawala wa Kiislamu na wasiokuwa wa Kiislamu, ni mdaiwa wa nguzo kuu ya fikra ya Kishia yaani Uimamu ambao ni moja ya zile Usul Ddin yaani Misingii ya Dini kwa mujibu wa itikadi ya Kishia. Moja ya sifa za kipindi hiki ni kukabiliwa fikra ya Kishia na changamoto ya fikra za Kimagharibi.

Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad mwanafalsafa mkubwa wa Kishia ni mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mshairi mahiri wa Kishia ambaye alihesabiwa kuwa nguzo muhimu ya maktaba ya Falsafa Isfahan Iran katika kipindi cha utawala wa Safavi nchini Iran. Kitabu chake mashuhuri na muhimu zaidi ni al-Qabasat na mwanafunzi wake mahiri ni Mulla Sadra. Mir Muhammad au Mir Damad kama anavyojulikana zaidi, alizaliwa mwaka 969. Baba yake ni Sayyid Muhammad Hussein Asterabadi na mama yake ni binti wa Muhaqiq Karaki au Muhaqiq Thani alimu na msomi mwingine mahiri wa Kishia. Mir Damad alikipitisha kipindi chake cha utoto chini ya malezi ya baba na mama waliokuwa na sifa njema na waliokuwa wamejipamba kwa maadili mema, taqwa na uchaji-Mungu. Kiujumla familia yake ilikuwa ya wasomi walioshikamana na elimu.
Baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi na ya awali alielekea katika mji wa Mash'had na kunufaika na bahari ya elimu ya wanazuoni na walimu waliokuwa stadi na mahiri katika zama hizo. Akiwa ameazimia kutekeleza malengo yake makubwa ya uhakiki, Mir Damad alifunga safari na kuelekea katika miji ya Qazvin, Harat na Isfahan ambayo katika zama hizo kila moja kati ya miji hiyo kilikuwa kituo muhimu cha elimu. Alipitisha kipindi cha miaka mingi akiwa katika miji hiyo.
Miongoni mwa walimu muhimu wa Mir Damad ni Sayyid Ali Amili, Abdul'Aali Amili, mjombake na Shekh Izzuddin Hussein Amili ambaye ni baba wa Sheikh Bahai. Inaonekana kuwa, safari za Mir Damad katika miji ya Qazvin, Harat na Mash'had zililenga kumfuata mwalimu wake yaani Sheikh Izzuddin ambaye kutokana na mazingira ya kisiasa na kijami ya wakati huo alibadilisha makazi yake mara kadhaa. Sheikh Bahai mtoto wa Sheikh Izzuddin ambaye tulimzungumzia katika kipindii chetu cha juma lililopita alikuwa rafiki wa karibu mno na wa kushibana wa Mir Damad, na wawili hao walikuwa wakinukuliana na kusimuliana visa vizuri na vya kuvutia.
Inasimuliiwa kwamba, siku moja wawili hawa walikuwa katika safari moja na Shah Abbas. Sheikh Bahai alikuwa na umbo jembamba na akiwa amepanda farasi wake alikuwa mbele amewatangulia Mir Damad na Shah Abbas. Tofauti na swahiba wake, Mir Damad yeye alikuwa na umbo kubwa na mnene na kadiri alivyojitahidi, farasi hakuweza kuongeza mwendo na kwenda haraka. Baada ya Shah Abbas kushuhudia mandhari ile akakusudia kuwatahini ili kujua ni kwa kiasi gani wanapendana au wanaoneana husuda. Hivyo akamkaribia Mir Damad aliyekuwa mnene na akiwa na tabasamu Shah Abbas akamushiria Sheikh Bahai na kusema: Bwana Mir, unaona huyu Sheikh hana adabu kabisa na ametupuuza sisi, ametangulia mbele na kutuacha nyuma na wala hana habari na sisi? Mir Damad akamjibu kwa kumwambia: Hapana, sivyo unavyodhania, Sheikh Bahai ni msomi mkubwa, na farasi ambaye amembeba mtu na shakhsia mkubwa kama huyu amepata hamasa na ndio maana anakwenda haraka. Shah Abbas akamtandika farasi wake ili aende mbio na amfikie Sheikh Bahai. Alipomfikia akamwambia: Nijuavyo mimi, wanafikra hujichunga katika suala la kula na hukinaika na chakula kidogo, lakini Mir Damad amekuwa na tamaa katika kula, mpaka amekuwa na umbo kubwa kama hili. Sheikh Bahai akavuta pumzi ndefu na kusema: Hapana, hivyo sivyo, Mir Damad ana tamaa ya elimu, na ukubwa wa mwili wake hauna uhusiano na kula sana. Farasi wake aliyempanda amechoka kutokana na kuwa amebeba kitu cha thamani ambacho hata milima haiwezi kuvumilia uzito wa elimu yake, na ndio maana unaona farasi wake anatembea kwa mwendo wa taratibu sana.

Kipindi cha kusoma Mir Damad huko Harat chini ya usimamizi wa mwalimu wake Sheikh Izzuddin, zilikuwa zama za utajiri wake wa kielimu. Ni baada ya kukamilisha kipindi hicho, ndipo alipotambuliwa kama msomi na mwanazuoni mahiri na kuwa mmoja ya wasomi wakubwa katika elimu za fikihi, falsafa na hadithi. Baada ya kuaga dunia Mfalme Tahmaseb na kuingia madarakani Shah Ismail wa Pili, mazingira kwa ajili ya Maulamaa wa Kishia yaligeuka na kuwa magumu kiasi, na shakhsia hawa wakubwa walikuwa wakifanya hima ya kuwa mbali na makao makuu ya utawala yaani mji wa Qazvin. Ni kutokana na sabahu hiyo ndio maana Mir Damad na Sheikh Bahai walihajiri Qazvin na kuhamia Isfahan na kujishughulisha na kufundisha wakiwa katika mji huo. Waliishi huko mpaka Shah Abbas aliposhika hatamu za uongozi na Isfahan kuchaguliwa kuwa mji mkuu. Kutokana na Shah Abbas kuwa na mapenzi makubwa na elimu na wanazuoni, kwa mara nyingine tena mazingira ya uhuru na usalama wa Maulamaa wa Kishia yakawa yameandaliwa.
Mir Damad amelea wanafunzi wengi na baadhi yao ni mashuhuri na watajika kama Mulla Sadra Shirazi, Abdul-Razaq Lahiji, Mulla Muhsin Feidh Kashani na Muhaqiq Khonsari.
Katika upande wa uandishi wa vitabu, msomi huyu ameacha na kuvirithisha vizazi vilivyokuja baada yake athari 50 zenye thamani ambapo baadhi yake zipo katika sura ya hati yake. Kitabu chake muhimu zaidi ni al-Qabasat. Vitabu vingine vya Mir Damad ni Taqdisat, Jadhawat na Sidratul Mutaha.
Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu kwa leo, sina budi kukomea hapa. Tukutane tena siku nyingine katika mfululizo wa vipindi hivi vya Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ambapo tutaendelea na maudhui hii historia ya Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad.