Nov 25, 2023 13:16 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia (88)-Mwisho

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Sehemu ya 88 kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya mwisho ya mfululizo huu kitaendelea kumzungumzia Imamu Khomeini. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki cha mwisho kabisa cha mfuululizo huu.

Baada ya kifo cha Ayatullah Boroujerdi, darsa za Ayatullah Khomeini zikaondokea kuwa, masomo ya daraja la kwanza katika Hawza. Wanachuoni wote walikuwa wakubaliana kwamba, Ayatullah Khomeini ndiye chaguo bora zaidi la kuwa Kiongozi wa Hawza na Umarjaa wa umma wa Mashia. Hata hivyo, Imamu Khomeini mwenyewe alikataa kukubali jukumu hilo zito.

Kwa kukosekana uongozi wa Marjaa, Mohammad Reza Shah Pahlavi mtawala wa Iran aliona ni fursa nzuri kwake ya kutekeleza mipango yake kupinga dini.

Imamu Khomeini

 

Katika hatua ya kwanza, aliondoa sharti la kuwa Mwislamu ili kushika baadhi ya nyadhifa za serikali ili aweze kuwajumuisha Wabaha'i katika serikali. Kwa mujibu wa mafundisho ya dini, wanazuoni walikuwa wakiamini kuwa, katika ardhi za Kiislamu ni lazima kutekelezwe sheria za Uislamu na kwamba usimamizi wa mambo haupaswi kuwa mikononi mwa wasiokuwa Waislamu, hivyo wakaupinga vikali mpango huo. Ili kuficha malengo yake makuu na kupotosha fikra za watu, Shah Pahlavi alianzisha uafiriti nao ulikuwa ni kutambua kwa mara ya kwanza katika historia ya Iran haki ya wanawake kupiga kura.

Shah alitaka kila mtu afikirie kuwa yeye anaitakia kheri Iran na wakati huo huo anahimiza kuungwa mkono tabaka fulani katika jamii yaani wanawake ili wanawake waunge mkono mpango wake huo na hivyo wasimame kukabiliana na matabaka mengine ya jamii.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa jeuri kamili mfalme Shah alikuwa amewatumia wanawake kama ngao dhidi ya masaibu yake, na Ayatullah Khomeini kamwe hakuwa tayari kuvumilia hadaa na udanganyifu huu mkubwa.

 

 

Imamu Khomeiini (MA)

Katika barua aliyoiandikia akiwahutubu wananchi, aliandika yafuatayo kuhusu nia ya nyuma ya pazia za Shah; “Uislamu haumzuii mwanamke kwa njia yoyote ile, bali katika nchi ambayo hata wanaume na wanazuoni wao hawana haki ya kutoa maoni yao, kutoa haki ya kupiga kura kwa wanawake si chochote zaidi ya udanganyifu wa kisiasa na hakuna lengo jingine isipokuwa kubadilisha maoni ya umma."

Kwa ufafanuzi huu, watu walisimama kuwaunga mkono wanachuoni. Hatimaye, baada ya miezi miwili, Shah na serikali yake walilazimika kulegeza kamba. Matokeo ya hatua ya kwanza ya Shah sit u kkwamba hayakuwa na manufaa kwake na wa wafuasi wake, bali kinyume chake, yalidhihirisha ukweli ambao yeye na watu wake waliokuwa karibu naye walikuwa wakiuogopa sana. ukweli huo ni nafasi ya kijamii na nguvu ya kisiasa ya Ayatullah Ruhullah Khomeini. Fakihi ambaye kidhahiri aliukataa Uongozi wa Umarjaa lakini kivitendo alikuwa amebadilika na kuwa kiongozi kamili wa Mashia na sasa watu wote walikuwa wakimuita kwa jina la Imam Khomeini.

Ilikuwa ni wakati tu makoloni ya Marekani yalikuwa kwenye vuguvugu la mapinduzi ya wananchi ambapo John F. Kennedy aliingia madarakani na kuwa rais wa Marekani. Kennedy aliamua kufanya mageuzi ili kuepuka hatari ya mapinduzi haya. Ilikuwa ni fremu ya mageuzi haya ambapo mfalme Shah wa Iran alitekeleza mpango wake wa pili. Mpango ambao baadaye aliuita "mapinduzi ya meupe".

 

Wasomi na wanazuoni walituma mwakilishi kwa mfalme ili kujua ukweli wa jambo hilo. Baada ya kutafiti na kuchunguza, walijua kwamba mpango huu ulikuwa ni pendekezo la Wamarekani, na kwa vile hawakuichukulia Marekani kama rafiki na muungaji mkono wa wananchi Waisamu wa Iran, waliupinga mpango huo. Lakini hii haikuwa sababu pekee ya upinzani wao, kwa maoni yao, mpango uliopendekezwa na Shah ulikuwa na matatizo ya kisheria na ulikuwa ukitekelezwa kwa pupa ya ajabu. Mpango wa Mapinduzi Meupe ulipigiwa kura Januari 1963 ilihali watu wengi hawakushiriki katika kura hiyo. Serikali ikatangaza kuwa wananchi walio wengi wameupigia mpango huo kura ya ndio. Rais Kennedy alikuwa wa kwanza kumpongeza mfalme Shah kwa kutekelezwa vyema kwa kura ya maoni.

Upinzani wa wanachuoni na watu dhidi ya mpango huo uliongezeka na Imam Khomeini akaitangaza sikukuu ya Nairuzi ya mwaka mpya wa Kiirani ni maombolezo ya kitaifa. Masiku hayo yalisadifiana na kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Sadiq (as) na hivyo wananchi wa Iran wa miji mbalimbali walikuwa wameeelekea Qom ili wakasikie kwa karibu ujumbe wa Maulamaa. Watu walikuwa wakikusanyika katika Chuo cha Feidhiya ingawa baina yao walikuwemo makachero wa Shah waliokuwa wamevaa nguo za kiraia. Hatimaye kikosi cha gadi ya taifa kikashambulia mkusanyiko huo na kufanya mauaji makubwa.

 

Mauaji ya Chuo Feidhiya yaliyyofanywa na vikosi vya usalama vya mfalme Shah

Miezi miwili baada ya tukio la Feidhiya watu walikuwa wakijiandaa kwa ajili ya maombolezo ya Ashura, lakini mfalme alikuwa ameruhusu kufanyika kwa maombolezo kwa masharti matatu; Kwanza, hakuna kitu kinachopaswa kusemwa juu ya mfalme. Pili, Israel isikashifiwe, na tatu, wazungumzaji wasiseme kwamba Uislamu uko hatarini.

Katika hali hiyo, Imam Khomeini alikwenda katika chuo cha Feidhiya ili akahutubie umati wa watu na kumtangaza Shah na Israel kuwa ndio sababu kuu ya matatizo yote ya taifa hili.

Imam Khomeini alihutibia kwa lugha kali na kwa ushujaa mkubwa na kumkosoa vikali mfalme Shah. Siku iliyofuata Imamu Khomeini akatiwa mbaroni. Siku iliyofuata wananchi wa Iran wakajitokeza katika maandamano kumuunga mkono kiongozi wao na huo ndio ukawa mwanzo wa kuelekea ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

 

Baada ya hapo, Imamu Khomeini alibaidishwa na kutiwa mbaroni mara kadhaa. Awali alipelekwa uhamishoni Uturuki kisha Iraq na baadaye Ufaransa. Baada ya miaka 14 ya kuwa uhamishoni hatimaye Imam Khomeini alirejea hapa nchini siku kumi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamuu na kuongoza harakati za mapinduzi ya wananchi yaliyopata ushindi 1979.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Hiki ndicho kipindi chetu cha mwisho cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Katika mfululizo huu tumewatambulisha zaidi ya Maulamaa 80 waliokuwa na mchango mkubwa katika Uislamu. Ni matumaini yangu kuwa mmenufaika vya kutosha, na kwa niaba ya wote waliofanikisha kukuleteeni kipindi hiki, jina langu ni Salum Bendera niliyekuwa mtayarishaji na msimulizi wa kipindi hiki ninakuageni nikitaraji kukutana nanyi katika kipindi kingine kipya juma lijalo Inshallah.

Wassalaam alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh