Nov 06, 2023 15:10 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (85)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tufungue ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia katika Uislamu Pamoja na mchango wao katika Uislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 85 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, ambaye hakuwa Marjaa Taqlidi wala hakufikia daraja ya ijtihadi, lakini daima alikuwa akifuatilia kufanya mambo makubwa.  Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Takriban sambamba na kuanza utawala wa Kipahlavi nchini Iran, alizaliwa katika moja ya vitongoji vya kusini mwa Tehran mtoto wa kiume. Mtoto huyu aliyezaliwa katika nyumba ya sharifu alipewa jina la Mujtaba. Baba yake ni Sayyid Javad Mir-Lohi aliyekuwa mmoja wa wanazuoni wa zama hizo ambaye alikuwa akifanya kazi katika idara ya mahakama mjini Tehran.

Mara nyingi Seyyid Javad alikuwa akizozana na wakubwa wake kazini kwa ajili ya kutetea haki za waliodhulumiwa, na hatimaye, moja ya hitilafu hizi zilisababisha ugomvi na kupigana ngumi. Hilo likamfanya atiwe mbaroni na kufungwa jela. Miaka mitatu baadaye, mwili usio na uhai wa baba ulitoka gerezani katika hali ambayo Seyyed Mojtaba alikuwa mtoto mdogo na hivyo akabakia yatima.

Ulezi na usimamizi wa Sayyid huyu yatima ulikabidhiwa kwa mjombake, na kuanzia hapo kila mtu alimfahamu kwa jina la ukoo la mama yake yaani, Navvab Safavi.

Picha za Sayyid Navvab Safavi katika marika mbalimbaali

Seyyid Mojtaba alipenda sana kusoma masomo ya dini, lakini mjomba wake alimpeleka katika shule ya viwanda ya Wajerumani ili kujifunza masomo ya kisasa. Seyyed Mojtaba aliachiwa na baba yake kumbukumbu ya shauku ya kujifunza elimu ya dini, na shauku hiyo ikampeleka kwenye Hawza (Chuo cha Kidini). Mbali na hilo aliachiwa pia kumbukumbu nyingine kutoka kwa baba yake ambayo daima ilikuwa ikidhihirika katika uwepo wake, nayo ni hamu ya kuendesha mapambano kwa ajili ya kupatikana kivitendo na kutawala sheria za Kiislamu.

Vita vya Pili vya dunia vilikuwa vimeanza na ukame na njaa vilikuwa vimehinikiza karibu miji yote ya Iran. Wananchi wa miji mbalimbali walikuwa wakijitokeza mitaani kila siku kufanya maandamano. Mnamo Desemba 17, 1942, Navvab Safavi, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 tu, aliwakusanya wanafunzi na kuwaita waandamane baada ya kueleza hali halisi ya jamii. Wanafunzi wenye njaa huku wakiimba "mkate na jibini", "tuna njaa, tuna njaa" walifunga shule na kuanza kuelekea kwa pamoja upande wa jengo la bunge.

 

Njiani, watu pia walijiunga nao na kidogo kidogo umati mkubwa ukawa umekusanyika ambao haungeweza kudhibitiwa tena. Mohammad Reza Shah Pahlavi, ambaye mwanzoni mwa utawala wake hakuwa akifurahishwa sana na Waziri Mkuu wake, Qawam al-Satna, alitumia maandamano hayo kama kisingizio cha kuleta ukosefu wa usalama na machafuko ili aweze kumuondoa Qawam katika nafasi yake.  Huu ulikuwa uzoefu wa kwanza wa Seyyid Mojtaba Navvab Safavi. Uzoefu mchungu ambao kama angejua kutoka nyuma ya pazia nini kinajiri, angeelewa jinsi nia yake safi ya kitoto ilivyochafuliwa kwa matarajio na malengo ya kisiasa.

Baada ya kumaliza masomo ya elimu ya sekondari, Seyyid Mojtaba aliajiriwa na Kampuni ya Mafuta ya Naftbadan. Akiwa huko pia, alikuwa akiwahamasisha wafanyakazi kudai haki zao. Tabia yake ilipelekea kutimuliwa kazi katika kampuni ya mafuta. Alichukua fursa hii na kwenda Najaf kuendelea na masomo ya dini, lakini nyakati zilimwita na kumpata aendesha mapambano. Mwaka mmoja baada ya kuondoka kwenda Najaf alipokea kitabu cha Ahmad Kasravi kilichojaa matusi dhidi ya Uislamu na Mashia.

Kasravi hata alifikia hatua ya kutambulisha tarehe 1 Desemba kama siku ya "sikukuu ya kuchoma vitabu" na akavichoma moto vitabu vya shakhsia wakubwa na mashuhuri wa Kiajemi kama vile Hafez na Saadi, vitabu vya dua na hata Qur'ani. Wanazuoni walita fatuwa ya kuritadi Ahmad Kasravi na Sayyid Navvab Safavi ndiye pekee aliyekuwa na ushujaa wa kutekeleze hukumu hii.

Sayyid Navvab Safavi

Seyyid Navvab alikuwa amekuja Iran kutekeleza hukumu hiyo, lakini alijua wazi kwamba, kwa mujibu wa Uislamu hatua ya awali ni kutoa mwongozo kwanza kwa Kasravi. Hivyo alipita katika miji mbalimbali na kutoa hotuba dhidi ya murtadi huyo ili kuwafanya watu watambue nia yake na alipofika Tehran alifanya mdahalo na Kasravi, lakini yote hayo hayakuwa na natija, kwani Kasravi hakuwa na nia ya kuacha chuki zake dhidi ya Uislamu.

Mnamo mwaka 1945, Vita vya Pili vya Dunia vilipoisha na Uingereza ikawa imeikalia kwa mabavu Palestina, Navvab Safavi, ambaye alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja tu, aliamua kuinuka na kuanzisha harakati kwa ajili ya kuanzisha utawala wa Kiislamu. Aliamini kwamba haiwezekani kukabiliana ubeberu wa kimataifa isipokuwa kwa kutumia harakati ya kimsingi na yenye mizizi na ili kufikia lengo hili, alianzisha kundi la Fada'iyan-e-Islam nchini Iran. Hata hivyo mtazamo wake wa kuanzisha utawala wa Kiislamu haukuwa ukilenga Iran peke yake.

Navvab Safavi alisafiri na kufanya juhudi nyingi za kuleta umoja baina ya Waislamu. Alikwenda Lebanon, Syria na Iraq, akakutana na Mfalme wa Jordan na akatoa hotuba huko Misri kwa mwaliko wa Harakati ya Ikkhwan al-Muslimiin. Mnamo 1954, alitoka Baghdad hadi Beirut na kutoka huko akaenda Baytul-Muqaddas kushiriki katika kongamano la kupinga Uzayuni.
 

 

Sayyid Navvab Safavi akiwa katika mkusanyiko na wenzake katika kundi la Fada'yan Islam

Akiwa huko alibainisha na kueleza mawazo yake kwa shauku na msisimko uleule kama kawaida na akawaita wote waliokuwepo kusali katika msikiti ulioko kilomita moja nje ya mji wa Quds. Maneno na mwenendo wake viliwafanya Wazayuni kuingiwa na hofu na mshangao. Hivyo wakiwa na silaha wakachukua hatua ya kuwazunguka waumini waliokuwa wakisali.

Navvab Safavi ameeleza maoni na mitazanmo yake kuhusu misingi ya kisiasa ya Uislamu na njia sahihi ya utawala katika kitabu kiitwacho "Jam'e va Hokomat Eslami" Jamii na Utawala wa Kiislamu, na akamuonya Shah wa Iran na serikali zingine ghasibu kwamba zisipotekeleza maamrisho ya Uislamu zitaangamizwa na watoto wa Uislamu wenye nguvu na waliojitolea muhanga. 

Mbinu ya Navvab Safavi ilikuwa ni kuwajulisha watu kwanza katika ngazi ya jamii na kisha kuwaelimisha watu katika ngazi ya serikali na kama hakukuwa na athari, aliwaonya viongozi na hatimaye hakuacha kuchukua hatua za kutumia silaha. Alikuwa akiamini kwamba, katika njia ya kufikia malengo, ima tutafanikiwa kufikia lengo au tutauawa shahidi".

Hatimaye upinzani wake dhidi ya ushawishi wa Marekani nchini Iran na kutangaza vita dhidi ya serikali ya wakati huo ya Iran, ulipelekea kutiwa mbaroni yeye na wenzake wa kundi la Fada'yan-e Islam na wakahukumiwa kunyongwa.

Wasia wa mwisho wa Navvab Safavi ulisema: Sisi tutauawa shahidi, lakini fahamuni kwamba, kutoka katika kila tone la damu yetu, watafunzwa na kulelewa Mujahidina na Iran itakuwa ya Kiislamu." Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwani mwaka 1979 mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipataa ushindi na mfumo wa Kiislamu ukaundwa hapa nchini, na Iran ikawa nchi ya Kiislamu.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh