Mahakama ya ICJ: Israel inapasa kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeitaka Israel ijiepushe kutumia sheria zake za upande mmoja maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na kuukosoa utawala huo ghasibu kwa kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo lililoharibiwa na vita la Gaza.
Katika maoni ya ushauri yaliyotolewa jana Jumatano, Mahakama ya ICJ ilisema kuwa Israel ambao ni "utawala ghasibu", haina mamlaka rasmi ya kuchukua maamuzi ya kisheria katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds kwa kuzingatia miswada ya unyakuzi iliyopasishwa jana na Bunge la Israel (Knesset).
Yuji Iwasawa, Mwanasheria Mashuhuri wa Japan na mkuu wa sasa wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) pia ameukosoa utawala wa Tel Aviv kwa kusitisha ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Iwasawa ameitaka Israel iwezesha programu zote za utoaji misaada kwa Wapalestina wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu akisema kuwa mahakama ya ICJ kwa kauli moja inaamini kuwa Israel ambao ni utawala ghasibu inawajibika kutekeleza majukumu yake ya kisheria.
Mwanasheria huyo Mashuhuri wa Japan pia ametangaza kuwa uamuzi wa pamoja umefikiwa kuhusu marufuku ya kutumiwa njaa kama silaha ya vita, akimaanisha kitendo cha Israel cha kulipiga marufuku kufanya kazi Ukanda wa Gaza shirika la UNRWA ambalo ni mtoaji mkuu wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo.
Amesema, Israel inapasa kukubali na kuwezesha mifumo ya utoaji misaada inayotolewa na Umoja wa Mataifa na vyombo vyake likiwemo shirika la UNRWA.