Rais Pezeshkian: Iran haitaki vita; mashinikizo ya kiuchumi yanalenga kuichafua serikali
-
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza tena msimamo wa Iran wa kuunga mkono amani, akisema kuwa nchi hii haijawahi kutaka kuanzisha vita, licha ya kukabiliwa na uhasama wa wazi kutoka kwa maadui zake.
Rais Pezeshkian ametoa kauli hiyo Jumatatu mjini Tehran wakati wa kikao kilichowakutanisha viongozi wakuu wa dini mbalimbali za Tauhidi pamoja na waumini wao. Mkutano huo uliandaliwa kuadhimisha miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Iran amesema: “Tangu mwanzo kabisa, tumekuwa tukisema wazi kwamba hatutaki vita; tunatafuta umoja, mshikamano, na kulitumikia taifa.”
Hata hivyo, Rais Pezeshkian amebainisha kuwa maadui wa taifa la Iran wamekuwa wakitumia shinikizo la kiuchumi kama chombo cha kisiasa, kwa lengo la kuzuia serikali kuwahudumia ipasavyo wananchi.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kuunda taswira ya “kutokuwepo kwa ufanisi” dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa nchi hiyo, ili kuudhoofisha mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa.
Rais huyo alikumbusha kuwa Iran imekabiliwa mara kwa mara na njama na mashinikizo kama hayo tangu siku za mwanzo za Mapinduzi ya Kiislamu, wakati taifa lilipoanza kusisitiza uhuru, kujitegemea, na kujitawala.
Kwa mujibu wake, maadui walifuata mkondo wa njama mbalimbali, ikiwemo kuchochea migawanyiko ya ndani, kupanga mapinduzi, na hata vita. Amesisitiza kuwa katika kipindi hicho, vijana wengi wa Iran walipoteza maisha yao wakilitetea taifa, wakisimamia haki na ukweli, na kuzuia kuporwa kwa ardhi ya Iran.
Rais Pezeshkian amesema kuwa dini zote za mbinguni zimebeba ujumbe wa pamoja wa kujizuia na migogoro, na zimeutambua ubinadamu wote kama umma mmoja, ambapo fadhila za juu kabisa zinapatikana katika nia njema, kauli njema, na matendo mema.
Akinukuu ujumbe wa Mtume Muhammad (SAW) wakati wa ushindi katika mji mtukufu wa Makka, Rais Pezeshkian amesitiza mafundisho yanayosema kuwa wanadamu wote ni sawa, na kwamba hakuna aliye bora kuliko mwenzake isipokuwa kwa uchamungu.
Katika muktadha wa kimataifa, rais wa Iran amekosoa vikali unafiki wa madola makubwa, akisema migogoro ya leo inaendeshwa na uchokozi na unyonyaji wa rasilimali na maslahi ya mataifa mengine.
Aliongeza kuwa kaulimbiu kama “demokrasia” na “haki za binadamu” mara nyingi hutumiwa vibaya kuhalalisha vitendo visivyo vya haki, hasa katika maeneo yenye rasilimali nyingi. Aidha, amelaani mashambulizi yanayowalenga raia wasio na hatia, wakiwemo watoto, wanawake, na wagonjwa, akiyataja kuwa kinyume na maadili ya kibinadamu na ya kidini.