Iran yamjia juu Makamu wa Rais wa ICJ kwa kuikingia kifua Israel
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemkosoa vikali Julia Sebutinde, Makamu wa Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kutokana na uungaji mkono wake wa wazi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi ameshutumu uungaji mkono usio na kifani wa Sebutinde, raia wa Uganda kwa Israel na kuutaja kama "ukiukaji wa kutisha wa maadili ya mahakama".
"Makamu wa Rais wa ICJ anaunga mkono wazi wazi Israel, utawala wenye kesi nyingi Mahakamani. Upendeleo huu wa wazi unadhoofisha uaminifu wa ICJ na unakiuka kanuni ya msingi ya mahakama kutoegemea upande mmoja," ameeleza Gharibabadi.
Katika matamshi aliyotoa mnamo Agosti 10, Sebutinde alisema, "Mola ananitegemea mimi kusimama upande wa Israel" na ishara za "nyakati za mwisho" "zinaonyeshwa Mashariki ya Kati".
Aidha mapema mwaka jana, Sebutinde alikuwa jaji pekee katika jopo la wanachama 17 la ICJ ambalo liliamua kuwa yumkini Israel ilikuwa ikifanya mauaji ya halaiki huko Gaza, ambaye alipiga kura dhidi ya hatua zote sita zilizopasishwa na mahakama hiyo.
Kadhalika mnamo Julai 2024, jaji huyo alikuwa tena mpinzani pekee wakati jopo la majaji 15 lilipogundua kuwa uvamizi wa Israel wa miongo kadhaa katika maeneo ya Palestina ulikuwa "haramu".
Vile vile Februari 2025, uchunguzi ulimshutumu Makamu wa Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa kughushi sentensi, neno kwa neno, katika maoni yake pinzani yaliyoandikwa mnamo Julai 19, 2024. Ilidaiwa kuwa, "angalau asilimia 32 ya mapingamizi ya Sebutinde yalighushiwa".