Iran inaweza kupunguza kiwango cha urutubishaji urani iwapo ‘vikwazo vyote vitaondolewa’
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136464-iran_inaweza_kupunguza_kiwango_cha_urutubishaji_urani_iwapo_vikwazo_vyote_vitaondolewa’
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa uwezekano wowote wa kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani ambayo sasa ni imefika hadi asilimia 60 utategemea kikamilifu iwapo vikwazo vyote dhidi ya nchi hiyo vitaondolewa.
(last modified 2026-02-10T07:16:51+00:00 )
Feb 10, 2026 07:16 UTC
  • Mohammad Eslami
    Mohammad Eslami

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa uwezekano wowote wa kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani ambayo sasa ni imefika hadi asilimia 60 utategemea kikamilifu iwapo vikwazo vyote dhidi ya nchi hiyo vitaondolewa.

Mohammad Eslami alitoa kauli hiyo mjini Tehran siku ya Jumatatu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pembeni mwa uzinduzi wa Maabara ya “Usalama wa Umeme na Mionzi.”

Akijibu tetesi za hivi karibuni kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa urani iliyorutubishwa na kupelekwa nje ya Iran, Eslami ametupilia mbali taarifa hizo, akizitaja kuwa ni “mada inayosukumwa na makundi mbalimbali ya shinikizo” dhidi ya Iran.

Eslami amefafanua kuwa: “Jambo kama hilo kimsingi halijawahi kuwa katika ajenda,” akiongeza kuwa wazo hilo huenda “lilitolewa na nchi au mtu binafsi aliyedhani lingeweza kusaidia.”

Iran na Marekani zilifanya mazungumzo mapya kuhusu nyuklia siku ya Ijumaa, huku pande zote mbili zikionyesha kuwa mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika katika siku za usoni.

Nchi hizo mbili zilikuwa zimeendesha awamu tano za mazungumzo kabla ya uchokozi wa Marekani na Israel mwezi Juni, hata hivyo mazungumzo hayo hayakuzalisha mafanikio yoyote ya maana.

Kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vyake vya nyuklia, Iran ilikuwa imerutubisha urani hadi asilimia 60, kiwango kinachozidi asilimia 3.67 kilichowekwa chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, ambayo sasa yalisambaratika baada ya Marekani kujiondoa.

Iran ilikuwa na takribani kilo 400 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu kabla ya uchokozi wa Marekani na Israel mwezi Juni uliopita, na hatima ya akiba hiyo imekuwa ajenda ya mjadala katika mazungumzo yanayoendelea.

Mkuu huyo wa nyuklia wa Iran pia amekosoa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa kunyamaza kwake kufuatia mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Amebainisha  kuwa Shirika hilo lina “wajibu ambao haujatekelezwa” wa kulaani mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyo chini ya usimamizi na uthibitisho wake yenyewe.