Nov 06, 2023 15:10 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (86)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 86 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Abul-Qassim Kashani.  Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Seyyed Abul-Qassim Kashani, ambaye ni mtoto wa Ayatullah Seyyed Mustafa Kashani, alizaliwa 1855 katika mji wa Tehran, Iran. Baba yake alikuwa mmoja wa wanazuoni wa Tehran na katika zama za utawala wa Naser al-Din Shah Qajar, na alikuwa na ushawishi mkubwa katika utawala huo. Seyyed Abul-Qassim alikuwa na umri wa miaka 16 wakati alipokwenda Najaf Ashraf na familia yake ili akaishi milele katikak mji huo. Alianza masomo yake huko Tehran na akaendelea nayo huko Najaf, Iraq na tangu enzi za ujana wake, alijulikana kwa umakini na upimaji mambo.

Seyyed Abul-Qassim Kashani alifikia daraja ya ijtihad akiwa na umri wa miaka 25, na wanazuoni wakubwa wa Najaf akiwemo Ayatullah Sadr mara nyingi walisifu nafasi yake ya kielimu na walimtaja kama "Mpasua Bahari ya Elimu" na "Ufunguo Katika Hazina Makini". Pia, Mirzaei Shirazi, Marjaa Mkubwa wa Mashia alitambua rasmi Umarjaa wake na kuthibitisha usahihi wa kumkalidi.

Ayatullah Seyyed Abul-Qassim Kashani, lakini alikuwa amerithi kutoka kwa baba yake ukubwa na adhama katika tabia na kuishi vyema na watu. Licha ya kuwa na daraja ya juu kielimu, akiwa katika mkusanyiko hakuchagua kukaa mahali maalumu na kama alivyokuwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwake yeye hakukuwa na tofauti yoyote katika mkusanyiko baina ya kukaa juu na chini.

Khushui na unyenyekevu vilikuwa dhahiri katika nafsi yake yote, na pamoja na elimu na hekima, pia alikuwa ameleta unyofu na usafi wa nia kwa kiwango cha juu kabisa. Lakini kujinyima huku na uchamungu, unyenyekevu, ikhlasi na uja hakukuishia kwenye mambo binafsi. Kama baba yake na waalimu wake, hakuwahi kuona kama mtu na jamii ni vitu viwili tofauti, na kwamba ubora na kukwea mwanadamu unawezekana tu kupitia mageuzi katika jamii. Ilikuwa ni kwa ajili hiyo ndipo tokea mwanzoni kabisa mwa ujana wake, roho ya mapambano dhidi ya dhulma ilihuika ndani yake na akafanya kazi kwa bidii katika kupambana na ukoloni na dhulma na kuboresha mambo ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, Ayatullah Kashani alikuwa na umri wa karibu miaka 35. Baada ya kukaliwa kwa mabavu Iraq na Waingereza, alipokea fatwa ya Jihad kutoka kwa Mirza Shirazi mkubwa na akayaita makabila na kaumu za Iraq kupigana na mkoloni Muingereza. Baada ya kushindwa kwa watu wa Iraq katika mapinduzi haya (mapinduzi ya 1920), Ayatullah Kashani alirejea Tehran lakini Uingereza haikusahau katu muqawama na kusimama kwake kidete dhidi ya upendaji makuu wa mkoloni huyo.

Miaka kumi na minane baadaye, wakati wakoloni walipopanga na kutekeleza Vita vya Pili vya Dunia kwa minajili ya kuwa na udhibiti zaidi kwa eneo la Mashariki ya Kati, moja ya malengo ya Waingereza ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa Ayatullah Kashani. Walikuwa wakitambua kwamba, kama Ayatullah Kashani atakuwa hai, angewasababishia matatizo mengi, hivyo chaguo bora kwao lilikuwa ni kumuondoa au kumweka kizuizini.

Mnamo mwaka wa 1945, sambamba na kufikia tamati Vita vya Pili vya Dunia, Wairani walishiriki katika uchaguzi wa duru ya 14 ya Bunge la Taifa, na wananchi wa Tehran walimpigia kura Ayatullah Kashani, lakini Waingereza ambao waliona uwepo wake unakinzana na maslahi yao, wakituumia ushawishi waliokuwa nao walimtia mbaroni na kumuweka kizuizini na hivyo kumzuia kushiriki katika vikao vya Bunge. Baada ya hapo, Ayatullah Kashani alionja mara nyingi adha za jela, mateso na maisha ya uhamishoni, lakini hakuacha mapambano dhidi ya dhulma na ukoloni.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, serikali za Russia na Uingereza kila moja ilitaka kupata hisa kubwa ya rasilimali za Iran na kulikuwa na ushindani baina yao katika suala hili, ushindani ambao haukuwa na natija nyingine kwa wananchi wa Iran ghairi ya uhohehahe na umasikini.

Hatimaye, Bunge lilipitisha sheria ambayo kwa mujibu wake serikali haikuwa na haki ya kutoa upendeleo kwa madola ya kigeni. Sheria hii ilisababisha baadhi ya mikataba ya mafuta ambayo ilifungwa na kusainiwa hapo kabla kutazamwa upya. Katika kipindi kifupi, Iran ilishuhudia Mawaziri Wakuu kadhaa, lakini hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyefanikiwa kuttekeleza haki za watu wa Iran.

Katika kipindi hiki, Ayatullah Kashani alibaidishiwa Lebanon, lakini bado alikuwa akifuatilia matukio ya Iran na kutuma matangazo kwa watu wa Iran. Ilikuwa ni kutokana na ufafanuzi na uwekeaji wazi mambo huo ambapo wanamapambano kadhaa walifanikiwa kuchaguliwa na kuingia katika bunge la 16, lakini mamlaka husika zilifanya njama na kuwazuia kushiriki vikao vya Bunge. Ufisadi wa serikali wa kujitakia na kutokuwa na uwezo wa kutetea haki na maslahi ya kitaifa ya wananchi wa Iran ndio uliosababisha wabunge kadhaa kuanzisha chama cha National Front ya Taifa na kuleta muswada wa kutaifisha sekta ya mafuta bungeni.

Ilikuwa ni wakati huu ambapo Ayatullah Kashani alirejea Iran na kwa kutumia ushawishi wake katika jamii, aliwaita watu wote kuunga mkono harakati hii mpya na kwa hotuba zake aliibua hamasa na vuguvugu kubwa miongoni mwa watu ambapo baada ya mapinduzi ya katiba hakushuhudiwa mtu mfano wake. Uungwaji mkono huo ndio uliopelekea Dk. Mohamed Mossadegh, mwanzilishi wa chama cha National Front, kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu, na kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Kimataifa wakoloni wakatakiwa kuondoka na kuheshimu haki za wananchi wa Iran. Huu ulikuwa mshindi mkubwa. Hata hivyo, wakoloni waliokuwa na chuki na hasama kubwa walimuonyeshea kidole cha lawama na chuki Ayatullah Kashani.

Baada ya ushindi wa wananchi wa Iran katika kutaifisha sekta ya mafuta, Mohammad Reza Shah Pahlavi, ambaye ufalme wake ulikuwa mdaiwa wa Waingereza, na chambilecho uso wa fadhila una haya, alimuuzulu Mossadegh na kumchagua Ahmad Qavam kutwaa nafasi hiyo. Ahmad Qavam, alikabiliwa na upinzani mkali wa wananchi na Maulamaa. Ayatullah Kashani aliingia uwanjani kwa mara nyingine tena na kuwalingania watu mapambano. Uwaziri Mkuu wa Qavam ulidumu kwa siku nne tu, baada ya hapo alilazimika kukubali matakwa ya wananchi na kuondoka madarakani. Mossadegh kwa mara nyingine tena akachukua usukani wa Waziri Mkuu wa Iran, lakini mara kiburi cha madaraka kilikuwa pamoja naye.

Kiburi hiki na kupenda jaha na madaraka vilisababisha kuibuka pengo kati yake na muungaji mkono wake mkubwa yaani Ayatullah Kashani. Wakati Ayatullah Kashani alipomuonya kuhusu mipango ya adui, hakulichukulia kwa uzito onyo hilo, na hatimaye mwaka 1953 Wamarekani walifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Mossadegh.

Harakati za Ayatullah Kashani hazikuishia nchini Iran tu bali zilikuwa zikijumuisha pia ulimwengu mzima wa Kiislamu na katika hili kwake yeye hakukuwa na tofauti baina ya Shia na Suni. Wakati utawala ghasibu wa Israel ulipotangaza uwepo wake, Ayatullah Kashani alitoa tangazo maalumu na kuwahutubu Waislamu wote ulimwenguni ambapo sambamba na kuyataja malengo ya kuasisiwa Umoja wa Mataifa kuwa ni urongo mtupu, aliashiria misimamo ya kidhulma ya umoja huo kuhusiana na Indonesia, Misri na Palestina. Hatimaye mwanazuoni huyu aliaga dunia mwaka 1962 baada ya kuvumilia machungu mengi ya gerezani pamoja na mateso na kuzikwa katika Haram ya Abdul-Adhim al-Hassan katika mji wa Rey.

Kwa leo nakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki. Tukutane tena wiki ijayo. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh