Nov 25, 2023 13:10 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia (87)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 87 ya mfululizo huu kitamzungumzia Imamu Ruhullah Khomeini msomi, mwanazuoni na Marjaa Taqlidi aliyeongoza harakati za wananchi wa Iran hadi kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.  Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Karne ya 14 Hijria kilikuwa kipindi cha misukosuko sana. Tawala za Uingereza, Marekani na Umoja wa Kisovieti kila moja ilikuwa ikifuatia kudhibiti rasilimali zaidi kutoka katika utajiri wa mataifa na kujaribu kupanua wigo wao wa ukoloni. Iran daima ilikuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa yakikodolewa macho ya ya tamaa na tawala hizi kutokana na kuwa na rasilimali nyingi na nafasi yake ya kijiografia. Eneo hili lilikuwa likihesabiwa kuwa sehemu ya kijiografia ya ulimwengu wa Kiislamu, eneo ambalo watu wake walikuwa na mapenzi ya Ahlul-Bayt, na ambao Shia na Sunni walikuwa wamejitolea kwa ajili ya watoto wa Mtume (SAW).

Miongoni mwa watu hao, daima walikuwepo wanazuoni ambapo kila mmoja wao alikuwa ni mshika bendera ya mapambano dhidi ya ukandamizaji wa wakoloni na madhalimu.

Yumkini takribani miaka 100 kabla ya kuzaliwa mwanazuoni huyu mwenye taathira, familia yake ilikuwa ikiishi Neyshabour. Mkubwa wa familia hiyo alikuwa Sayyid Haidar ambaye akiwa na lengo la kwenda kueneza Uislamu alielekea Kashmir akiwa pamoja na familia yake. Akiwa katika njia ya kupambana na ukoloni wa Uingereza nchini India alijitolea maisha na uhai wake baada ya kuuawa shahidi.
Baadaye mmoja wa watoto wake aliyejulikana kwa jina la Sayyid Mustafa alielekea Iraq na kujifunza elimu mbalimbali kwa Mirzaei Shirazi Mkubwa, mwanazuoni ambaye ndiye aliyetoa fatuwa ya kuharamisha matumizi ya tumbaku.

Nyumba ya Sayyid Mustafa katika mji wa Khomein

Baada ya Mirzaei Shirazi Mkubwa kuaga dunia, Sayyid Mustafa alikuja Iran kwa mwaliko wa wananchi wa Arak na kuishi katika eneo ambalo baadaye lilikuja kujulikana kwa jina la Khomeini.

Katika zama hizo, Harakati ya Kupigania Katiba nchini Iran haikuwa imetokea na watawalaa wa ukoo Qajar ndio waliokuwa wakitawala nchini Iran.

Ufisadi na kutokuwa na ustahiki ukoo wa Qajar ulifikia hatua ambayo walikuwa wakikodisha nyadhifa za utawala wa maeneo mbalimbali wakiwa na lengo la kuhifadhi nyadhifa zao fedha zilizokuwa zikitakiwa na wanamfalme wa Qajar walikuwa wakizichukua kwa nguvu na unyang'anyi kutoka kwa wananchi. Aidha kupitia hilo watawala hao walikuwa wakijilimbikizia utajiri. Katika mazingira haya Sayyid Mustafa hakuwa na budi isipokuwa kuendesha mapambano ya wazi dhidi ya dhulma hii na ili kufanikisha hilo kuna wakati alilazimika kubeba silaha na kuendesha mapambano dhidi ya magenge mbalimbali katika eneo la Khomein. Mapambano hayo ndio yaliyopelekea Sayyid Mustafa auawe shahidi akiwa na umri wa miaka 47.

Ruhullah Khomeini katika kipindi cha  utoto

 

Mwanawe wa mwisho alikuwa na miezi mitano tu wakati yeye anaaga dunia na hivyo hakuonja kabisa ladha ya kuwa na baba. Mtoto huyu si mwingine bali ni Ruhullah Khomeini ambaye baadaye alikuja kuitikisa dunia alipoongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 yaliyohitimisha utawala dhalimu wa Shah. Mtoto Ruhullah daima alikuwa akisikia simulizi kutoka kwa mama, ami na kaka zake kuhusiana na ushujaa na moyo wa kupigania uadilifu aliokuwa nao baba yake na kadiri alivyokuwa akikukua ndivyo alivyokuwa akiondokea kumpenda zaidi marehemu baba yake.

Wakati wananchi wa Iran wakiwa katika joto la mapinduzi ya katiba, "Ruhullah" alikuwa na umri wa miaka mitano tu na alikuwa kwenye joto na shauku ya kawaida ya kwenda shule. Alisoma masomo ya msingi msingi, sayansi ya kisasa na baadhi ya masomo ya Hawza kutoka kwa walimu na wasomi wa eneo la Khomein.

Sayyid Ruhullah Khomeini katika enzi za ujana wake

 

Katika kipindi hicho, aliendelea kushuhudia ukatili wa watawala wa eneo hilo na mara kwa mara aliona jinsi waasi na wauaji wanavyopora mali za watu wa mjini na mashambani na kuwanyima usalama wananchi.

Katika hali kama hiyo, nyumba ya mababu ya Seyyed Ruhollah iligeuka na kuwa kimbilio la watu wasio na kimbilio. Aliona matatizo na mazonge ya watu kwa ukaribu, na licha ya umri wake mdogo, nyakati fulani ilimbidi kuchukua silaha pamoja na watu wengine wa familia ili kupigana na waasi.

 

Seyyed Ruhollah alikuwa bado mwanzoni mwa rika la ujana wakati mataifa makubwa yalipopuliza tarumbeta la Vita vya Kwanza vya Dunia na kuongeza ukatili mwingine kwa kile kilichokuwa tayari kimefanyika. Urusi na Uingereza ziliingia Iran na kuweka majeshi yao kando kando ya miji ya Qom na Arak.

Nyumba ya Imamu Khomeini katika mji wa Qom

 

Makazi ya Seyyed Ruhollah yalikuwa sasa yamekuwa eneo la vita kamili na alikuwa anajua matukio yote. Matukio hayo yote yalichangia katika kuunda shakhsia yake na kumpelekea kutafuta njia za kuwatetea wanyonge na mustadhaafina na hivyo kubadilisha hali iliyokuwapo.

Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia, Seyyed Ruhollah alikwenda katika Hawza ya mji wa Arak hapa Iran kwa ajili ya kuendelea na masomo yake kwa Abdul Karim Hairi Yazdi. Miaka miwili tu baada ya mapinduzi ya Reza Khan na kutoweka kwa ukoo wa Qajar, Ayatollah Hairi Yazdi alikwenda Qom kuanzisha Hawza yaani Chuo cha masomo ya dini na Ruhollah Khomeini alifuatana naye na kuanza kuishi katika mji wa Qom.

Ruhollah, ambaye sasa alikuwa kijana wa miaka ishirini, alikutana na kufahamiana na walimu wengi huko Qom ambapo sambamba na kozi za masomo ya dini, alijifunza pia elimu zingine kama vile hisabati, jiometri na falsafa.

Kati ya masomo haya yote, alivutiwa na sana elimu ya Irfan na kila mara alikuwa akitafuta mtu wa kumwongoza kufikia kilele cha elimu ya Irfan. Hatimaye, katika nyumba ya mmoja wa wanachuoni, alikutana na Khatibu kutoka Tehran aitwaye Ayatollah Shahabadi.

Seyyed Ruhollah alifahamu katika siku ya kwanza tu ya masomo kwamba, huyu ndiye mwalimu aliyekuwa akimtafuta kwa miaka mingi. Alisoma elimu ya Irfani kwa Ayatollah Shahabadi kwa muda wa miaka sita na akaondokea kuvutiwa mtu na mwalimu huyu.

Kana kwamba alimuona baba yake katika haiba na muonekano wa mwalimu huyo. Uleule ushujaa na moyo wa mapambano ambao alikuwa ameusikia mara nyingi kutoka kwa wengine, sasa ulikuwa umejidhihirisha mbele ya Ayatullah Shahabadi. 

Ayatullah Shahabad

Hatimaye mwaka 1934 Ruhullah Khomeini akafikia daraja ya Ijtihadi. Kutokana na kuwa asili yake ilikuwa Khomein akaondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sayyid Ruhullah Khomeini ambapo mahali pake pa kufundishia pakawa sehemu ya mkusanyiko mkubwa wa wanafunzi. Nii katika miaka hii ambapo alisambaza kitabu chake cha kwanza. Kitabu hiki cha kiirfani kilihusiana na siri za Sala, siri ambazo si kila mtu anazifikia na kuzifahamu.

Seyyed Ruhollah Khomeini alikuwa na umri wa takriban miaka thelathini na mitano wakati ulimwengu ulipohusika kwa mara nyingine tena katika vita vikubwa na matukio yale yale ya utotoni yalijirudia tena mbele ya macho yake.

Baada ya vita, takribani hakuna kilichokuwa kimesalia kwa Iran na uhuru wake, na serikali ya kidikteta ya Pahlavi ilikuwa ni mwanasesere na kibaraka tu wa Marekani.

Kwa upande mwingine, Hawza ilikuwa imempoteza kiongozi wake, Ayatollah Hairi, na watu pia walikuwa wakipitia hali ngumu katika jamii. Katika hali kama hiyo, Seyyid Ruhollah na marafiki zake waliikuwa wakiamini kwamba, kuleta umoja na mshikamano katika jamii ni miongoni mwa mahitaji ya mwanzo ya jamii, kwa sababu ni hapo tu ndipo umma ungeweza kurejesha uwezo wake wa awali na kusimama dhidi ya utakaji makuu na kuwa kimbilio la watu wanyonge.

Walifanya jkuhudi kubwa sana hadi hatimaye Ayatollah Boroujerdi akakubali kuchukua jukumuu la uongozi wa Hawza ya Qom na baadaye kidogo, watu wote wakamtambua kuwa Marjaa mkuu wa Mashia ulimwenguni.

Katika miaka yote hii, Ruhullah Khomeini daima alikuwa mshauri na mwaminifu wa Ayatollah Borujerdi na alimwakilisha katika masuala mengi.

Ayatollah Borujerdi

 

Kuwepo kwa Ayatollah Boroujerdi kulifanya utawala wa Pahlavi kuachana na mipango yake mingi ya Marekani, lakini mwaka 1961 wakati Ayatollah Boroujerdi alipofariki dunia, Mohammad Reza Shah alifikiri kwamba angeweza kutimiza ndoto zilizosumbua za Wamarekani nchini Iran. Baada ya hayo, shughuli za kisiasa na kijamii za Ayatollah Seyed Ruhollah Khomeini ziliingia katika hatua mpya. Mapambano yake ndio kwanza yalikuwa yameanza.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia ukingoni tukutane tena juma lijalo ambayo itakuwa sehemu yetu ya mwisho ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags