Netanyahu amramba miguu Trump amuokoe na kitanzi cha kesi mahakamani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133872-netanyahu_amramba_miguu_trump_amuokoe_na_kitanzi_cha_kesi_mahakamani
Duru za kuaminika za Marekani na Israel zimefichua kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu amemuomba kwa kumsisitiza rais wa Marekani, Donald Trump afanye kila awezalo kuhakikisha kuwa anafutiwa kesi zake za ufisadi.
(last modified 2025-12-03T06:37:46+00:00 )
Dec 03, 2025 06:37 UTC
  • Netanyahu amramba miguu Trump amuokoe na kitanzi cha kesi mahakamani

Duru za kuaminika za Marekani na Israel zimefichua kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu amemuomba kwa kumsisitiza rais wa Marekani, Donald Trump afanye kila awezalo kuhakikisha kuwa anafutiwa kesi zake za ufisadi.

Shirika la Habari la Fars limezinukuu duru hizo za kuaminika zikisema katika taarifa yao ya leo Jumatano kwamba waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amemsihi Donald Trump amsaidie kupata msamaha katika kesi za ufisadi.

Kwa upande wake, tovuti ya habari na kiuchambuzi ya Axios nayo imewanukuu maafisa wa Marekani na Israel wakidhitibisha habari hiyo na kusema: "Netanyahu amemwomba Trump msaada zaidi katika ombi lake la msamaha wa kesi za ufisadi."

Duru hizo za kuaminika za Marekani na Israel ambazo zimekataa kutaja majina na vyeo vyao kwa sababu si wasemaji rasmi, zimeitaarifu tovuti ya Axios kwamba: "Trump amemwambia Netanyahu kuwa anaamini msamaha utatolewa, lakini yeye Trump hatojitolea kuchukua hatua yoyote maalumu ya kufanikisha msamaha huo."

Kwa mujibu maafisa hao wa Israel na Marekani, inaonekana kwamba Trump amemshinikiza Netanyahu kubadilisha mwelekeo wake huko Ghaza na Syria badala ya kushikilia tu kusaidiwa kupata msamaha wa makosa yake ya ufisadi yeye na familia yake.

Ripoti hiyo imeendelea kuksema: "Trump amemwambia Netanyahu kwamba anahitaji kuwa mshirika bora katika kutekeleza makubaliano ya amani."

Wakati huo huo, Channel ya 12 ya televisheni ya Israel imeripoti kwamba Trump amemuuliza Netanyahu kwa nini Israel iliwaua wanachama wa Hamas waliokuwa wamenaswa kwenye handaki?