Umoja wa Mataifa: El Fasher Sudan kumefanyika jinai za kivita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133870-umoja_wa_mataifa_el_fasher_sudan_kumefanyika_jinai_za_kivita
Mratibu wa Msuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan amesema mapema leo Jumatano kwamba maeneo mengi ya makazi ya raia nchini humo yamezingirwa na haiwezekani kuyafikishia misaada.
(last modified 2025-12-03T06:36:34+00:00 )
Dec 03, 2025 06:36 UTC
  • Umoja wa Mataifa: El Fasher Sudan kumefanyika jinai za kivita

Mratibu wa Msuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan amesema mapema leo Jumatano kwamba maeneo mengi ya makazi ya raia nchini humo yamezingirwa na haiwezekani kuyafikishia misaada.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; Bi Clementine Nkweta-Salami, Naibu wa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, ni jambo lisilo na shaka kwamba kumetokea uhalifu na jinai za kivita huko El Fasher, magharibi mwa Sudan.

Akihojiwa na televisheni ya Al Jazeera, Nkweta-Salami amesema: "Tunachokabiliana nacho El Fasher ni eneo la uhalifu na jinai za kivita na tunachukua tahadhari ili kulinda usalama watu wowote wanaoingia humo."

Amesema kwamba hadi hivi sasa Umoja wa Mataifa haujakidhi mahitaji ya wakimbizi wa vita wa Sudan kwa sababu kuna vijiji vilivyozingirwa na hawawezi kufikia kwa ajili ya kutoa msaada.

Wakati huo huo, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza Kuu la kijeshi la uongozi wa Sudan kwa mara nyingine amesema kuwa, hatokubaliana na suluhisho lolote ambalo halitapelekea kuvunjwa na kupokonya silaha Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.

Kamanda huyo wa jeshi la Sudan SAF ameongeza kuwa, vita vimewaathiri watu wote wa Sudan na mateso na maafa makubwa yanaendelea hivi sasa katika mji wa El Fasher ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na wakati huo huo amesisitiza kwamba, suluhisho pekee la mgogoro wa Sudan ni kuangamizwa RSF.

Ameongeza kuwa, watu wote wa Sudan wameonja uchungu wa vita na kuongeza kwa kusema: "Ninatoa mwito kwa raia wote ambao wanaweza kubeba silaha kujiunga na jeshi la SAF kupigana na wanamgambo wa RSF."