Nov 09, 2021 23:17 UTC
  • Jumatano tarehe 10 Novemba 2021

Leo ni Jumatano tarehe 4 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Novemba 10 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1270 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Haram ya Sayyid Abdul Adhim

Siku kama ya leo, miaka 930 iliyopita alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’

Miaka 538 iliyopita muwafaka na leo, alizaliwa Martin Luther mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani. Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusuiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi ya juu wa kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa kanisa. Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki kwa kuifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani na akaanzisha harakati ya kiprotestant dhidi ya kanisa hilo.

Martin Luther

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba mwaka 1899, kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofahamika kwa jina la Brumaire nchini Ufaransa. Brumaire lilikuwa jina la mwezi wa pili katika kalenda ya mapinduzi ya Ufaransa ambao unaenda sambamba na mwezi wa Novemba kwa kalenda ya Milaadia. Siku hiyo Napolione Luis Banaparte ambaye alikuwa akijihusisha na ushindi dhidi ya nchi za kaskazini mwa Afrika na Misri, alirejea kwa siri nchini kufuatia mwaliko wa kiongozi mmoja wa utawala wa Ufaransa. Aidha Luis Banaparte kwa kutegemea uungaji mkono wa askari jeshi na Bunge la nchi hiyo alifanikiwa kupindua utawala uliokuwepo nchini Ufaransa na kuanza kuiongoza rasmi nchi hiyo.

Luis Banaparte

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba 1912, Morocco alianza kukoloniwa na Ufaransa na Uhispania. Kabla ya hapo nchi hiyo inayopatikana kaskazini mwa Afrika ilikuwa ikikaliwa na madola mbalimbali kama vile dola la Othmania, Roma na Italia. Baadaye Uhispania na Ufaransa zilianza kukosana na muungano wao katika kuikoloni Morocco ukavunjika. Ufaransa iliendelea kuikoloni nchi hiyo na baada ya muda usio mrefu, wananchi wakaanzisha mapambano yao dhidi ya Wafaransa. Hatimaye mapambana hayo yalipata ushindi na Morocco ikajipatia uhuru wake 1956.

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Dakta Sayyid Hussein Fatimi Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq aliuawa kwa kupigwa risasi na vibaraka wa utawala wa Shah nchini Iran. Dakta Fatimi kabla ya hapo alikuwa amehukumiwa kunyongwa na mahakama moja ya kijeshi ya kimaonyesho ya utawala wa Shah huku akiwa mgonjwa sana. Baada ya mapinduzi ya Marekani ya tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsiya hapa nchini na baada ya kujiuzulu Dakta Musaddiq, Dakta Sayyid Hussein Fatimi alikuwa akisakwa na vibaraka wa utawala wa Shah na alikuwa akiishi kwa kujificha. Alikamatwa na kunyongwa katika siku kama ya leo.

Dakta Sayyid Hussein Fatimi katika mahakaa ya kijeshi

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 10 Novemba 1964, Leonid Brezhnev alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha CPSU katika Urusi ya zamani na hivyo kuchukua rasmi jukumu la kukiongoza chama hicho. Brezhnev aliendelea kushikilia cheo hicho cha ukatibu mkuu hadi kifo chake mwaka 1982. Katika kipindi chake cha uongozi, Umoja wa Usovieti ulipata nguvu zaidi kijeshi lakini pia ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Viongozi wa kikomunisti waliokuja baada yake walisema matatizo aliyoyaacha Leonid Brezhnev ndiyo yaliyopelekea Umoja wa Usovieti kuporomoka na kuvunjika kabisa mwaka 1991.

Leonid Brezhnev

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua uzayuni (Zionism) kuwa ni aina fulani ya ubaguzi wa kizazi. Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ni ndio kizazi bora zaidi ya wengine wote duniani. Kwa mujibu wa fikra hiyo Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi dunia na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na nchi yao.

Bendera ya Wazayuni

Na tarehe 10 Novemba mwaka 1981 wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Ufaransa na Iraq zilitiliana saini mkataba wa mauzo ya silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni moja. Mkataba huo ulikuwa moja kati ya mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha baina ya Ufaransa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran. Ufaransa ilikuwa bega kwa bega na utawala wa Saddam Hussein tangu mwanzoni mwa mashambulizi na uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilihesabiwa kuwa muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa utawala wa dikteta Saddam Hussein baada ya Russia. Silaha hizo zilijumuisha ndege za kisasa za kivita, makombora ya aina mbalimbali, vifaru, mizinga na aina nyingine za zana za kivita. Ufaransa pia ilimsaidia Saddam Hussein katika kutengeneza silaha za kemikali. Vilevile iliupatia utawala wa Iraq mkopo wa dola bilioni 5 wakati wa vita vyake dhidi ya Iran na imekataa kulipa deni la dola bilioni moja kwa Iran.

Tariq Aziz na François Mitterrand