Alkhamisi tarehe 11 Novemba 2021
Leo ni Alkamisi tarehe 5 Rabiuthani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Novemba 2021.
Miaka 176 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarahe 5 Rabiuthani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran. Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasiruddin Shah Kajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabiri. Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapishwa hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo likaendelea kuchapishwa kwa majina tofauti.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.

Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio, viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.