Jumapili, tarehe 14 Novemba, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 8 Rabiuthani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Novemba 2021.
Siku kama ya leo miaka 1211 iliyopita alizaliwa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Askari alilazimishwa na watawala wa Bani Abbas kwenda uhamishoni huko Samurra akiwa pamoja na baba yake na kufaidika na elimu ya Imam Hadi kwa kipindi cha miaka 13. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha karibu miaka sita baada ya kuuawa shahidi baba yake. Sehemu ya umri wake wa miaka 28 iliishia katika jela za watawala madhalimu wa Bani Abbas au akiwa uhamishoni na chini ya udhibiti wa watawala hao. Hata hivyo mtukufu huyo hakuacha kueneza maarifa sahihi ya Uislamu na kulea kizazi cha wanazuoni hodari.

Katika siku kama ya leo miaka 1086 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Firas al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Firas al-Hamdani alikuwa mpiganaji na miongoni mwa watu wa karibu kwa Seif ad-Dawlah mtawala wa Halab na alikuwa miongoni mwa makamanda wake.
Siku kama ya leo miaka 488 iliyopita, ardhi ya Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania. Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu. Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita mwafaka na tarehe 22 Aban mwaka 1344 Hijria Shamsia, alifariki dunia mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani, Said Nafisi akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kupata elimu ya upili, Nafisi alielekea Ufaransa kwa ajili ya elimu ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake huko Ufaransa alirejea Iran na kufunza katika vyuo vikuu hapa nchini. Said Nafisi ameandika na kutarjumu vitabu zaidi ya 180 ikiwemo kamusi ya lugha ya Kifaransa na Kifarsi.
Miaka 305 iliyopita katika siku kama ya leo, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani. ***
Katika siku kama ya leo miaka 224 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia. Baada ya kufanya utafiti mkubwa hatimaye aliandika kitabu cha mijadala mitatu kuhusiana na misingi ya elimu ya utambuzi wa ardhi alichokipa jina la Principles of Geology.
Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.
Miaka 132 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri alizaliwa. Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa. Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri. ***