Nov 16, 2021 22:57 UTC
  • Jumatano, Novemba 17, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Saba Rabiuthani 2443 Hijria sawa na tarehe 17 Novemba mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1223 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu. Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid' na 'Siyarul-A'amaal.' Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.

Siku kama ya leo miaka 835 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alipta elimu za awali katika mji alikozaliwa akiwa bado kijana, na baadaye alifanya safari katika maeneo mbalimbali na kukutana na wataalamu wa sheria na fiqhi ya Kiislamu na wanahistoria wakubwa na kufaidika na elimu yao. Kwa muda mrefu Ibn Khallikan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo na alibobea sana katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulioko Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi. Miongoni mwa vitabu vyake ni kile cha "Wafayatul Aayan".

Ibn Khallikan

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia. Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18 sambamba na kujenga kiwanda cha ufumaji. Katika kiwanda chake hicho kwa mara ya kwanza alianza kuboresha hali ya afya na ustawi wa wafanyakazi barani Ulaya kwa kupunguza masaa ya kazi kutoka masaa 14 kufikia masaa 10.

Robert Owen

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200. Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia Afrika Kusini.

Ferdinand de Lesseps

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Libya ulianza tena. Uhusiano huo ulikuwa umekatika kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hilo lilitokana na hatua ya Kanali Muammar Gaddafi Kiongozi wa wakati huo wa Libya ambaye alikuwa akiutambua utawala wa kifalme wa Kipahlavi hapa nchini kuwa, ulikuwa ukifungamana na ubeberu wa Marekani ambao ulikuwa ukitanguliza mbele maslahi na manufaa ya Magharibi na utawala vamizi wa Israel mbele ya maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.