Jumanne tarehe 14 Disemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 9 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 14 Disemba mwaka 2021.
Tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 463 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadruddin Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadrul Muta'allihīn au Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu. Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha. Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. al Mabdau Wal-Maad, Zadul Musafir na Mutashaabihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadrul-Muta'allihīn.
Miaka 216 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na 14 Disemba 1805, iligunduliwa nishati ya joto ya makaa ya mawe na George Branclon, mhunzi kutoka Uingereza. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya joto, ilipatikana katika bandari moja iliyoko Uingereza.
Miaka 110 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1911, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ya kinyama ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967.
Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na Waserbia.
