Dec 26, 2021 02:35 UTC
  • Jumapili 26 Disemba 2021

Leo ni Jumapili tarehe 21 Jamadil Awwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Disemba mwaka 2021.

Miaka 1122 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijiria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qiravani, katika mji wa Shirvan ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo alijulikana kwa jina maarufu la Ibn Jazzar, na alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu mema na aliandika kitabu kiitwacho "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika karibu vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.

Ibn Jazzar

Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi mashuhuri kwa lakabu ya Sayyid al-At’baa mmoja wa matabibu mahiri wa Iran alifariki dunia. Alizaliwa katika mji wa Tabriz nchini Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali ya kidini alisafiri na kuelekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Sayyid Ali Mar’ashi alisoma kwa kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Najaf na kurejea katika mji aliozaliwa akiwa na shahada ya Ijtihadi. Kutokana na mapenzi yake makubwa na elimu ya tiba alielekea katika mji wa Isfahan na kusoma taaluma hiyo kwa muda wa miaka 15. Alimu huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa ambapo Tarikh Tabriz na Sharh Tib al-Nabbi ni baadhi tu ya vitabu vyake muhimu.

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan. Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi. Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan.

Shambulizi la Jeshi Jekundu la Urusi huko Afghanistan

Tarehe 5 Dei mwaka 1382 Hijria Shamsia yaani siku kama hii la leo miaka 18 iliyopita, mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 6.8 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika mji wa Bam kusini mwa Iran na maeneo ya kandokando yake. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu sehemu kubwa ya mji huo na kusababisha vifo vya watu elfu 41. Makumi ya maelfu ya watu wengine pia walijeruhiwa. Maafa ya mtetetemo huo wa ardhi yalikuwa makubwa mno kwa kadiri kwamba baadhi ya jumuiya na taasisi za kimataifa zilijiunga na wananchi na serikali ya Iran katika kutoa misaada ya dharura kwa waathiriwa. Mbali na hasara za nafsi na vifo vya maelfu ya watu, mtetemeko wa ardhi wa Bam ulisababisha pia hasara kubwa za kiuchumi na kuharibu jengo la kale la Arge Bam.

Bam

Na katika siku kama ya leo miaka 17 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami. Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo. Mawimbi ya Tsunami yaliyosababishwa na mtetemeko huo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola.

AIR