Dec 30, 2021 03:19 UTC
  • Alkhamisi tarehe 30 Disemba 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 30 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Muawiya bin Yazid, Khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Umayyah aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia baba yake yaani Yazid bin Muawiya. Hakuwa na hamu ya kuendelea kuongoza kwa sababu alikuwa akitambua kwamba, Ahlul Bait wa Mtume (a.s) ndio waliostahiki jambo hilo. Muawiya bin Yazid anayejulikana kama Muawiya wa Pili, alitoa hotuba na kulaani vita vya babu yake, yaani Muawiya bin Abi Sufyan, dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na vita vya baba yake, yaani Yazid dhidi ya Imam Hussein bin Ali (a.s) na kuwasifu Ahlul Bait (a.s).

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo.

Jinai za Wazayuni

Miaka 43 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo.

Shapour Bakhtiar

Tarehe 30 Disemba miaka 15 iliyopita Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraq, alinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi ikiwemo Marekani. 

Saddam Hussein

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba, yaani miaka 12 iliyopita, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. Kwa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali".

AIR