Jan 24, 2022 22:57 UTC
  • Jumanne tarehe 25 Januari 2022

Leo ni Jumanne tarehe 22 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 25 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1052 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa mashairi wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj. Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq na alijikita katika taaluma ya mashairi akiwa bado kijana na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo. Alitunga mashairi mengi yanayowaenzi na kuwasifu Ahlul bait wa Mtume (saw) na kuwashambulia wapiznani wa Uislamu na Mtume. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yenye juzuu kumi inayohifadhiwa katika maktaba mbalimbali duniani.

Katika siku kama ya leo miaka 566 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. 

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani.

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Tarehe 5 Bahman miaka 43 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji. Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran. Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah. Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku  kama ya leo miaka 16 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.