Jumatano tarehe 26 Januari 2022
Leo ni Jumatano tarehe 23 Jamadithani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Januari 2022.
Miaka 199 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Jenner alizaliwa mwaka 1749. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. mwaka 1979 maradhi hayo yalitokomezwa kabisa duniani.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita mfumo wa Jamhuri ulitangazwa nchini India na siku hii ikapewa jina la Siku ya Kitaifa ya India. Baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza Jawaharlal Nehru alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu huku Rajendra Prasad akichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa mfumo wa India, wadhifa wa urais ni wa kiheshima tu na Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali. India ina jamii ya karibu watu bilioni moja na milioni hamsini na ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi duniani baada ya China.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, kilianza kipindi cha Uwaziri Mkuu wa Amir-Abbas Hoveyda aliyekuwa mmoja kati ya watu waliokuwa watiifu kwa utawala wa kifalme wa Shah hapa Iran. Baada ya kunyongwa Hassanali Mansour, Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala wa Shah, Amir-Abbas Hoveyda aliyekuwa Waziri wa Hazina katika Baraza la Mawaziri la Mansour aliamriwa kuunda serikali akiwa Waziri Mkuu. Amir-Abbas Hoveyda alishikilia wadhifa huo kwa takribani miaka 13 hadi mwaka 1977.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, kundi lililokuwa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu lililojulikana kwa jina la Muungano wa Wakomonisti, lilishambulia mji wa Amol wa kaskazini mwa Iran. Kundi hilo lilikuwa likijidanganya kwamba, eneo hilo litakuwa kituo chao cha mashambulio yao ya baadaye kaskazini mwa Iran. Vikosi vya wapiganaji na wananchi wanamapinduzi wa mji huo kwa muda mfupi walifanikiwa kuzima mashambulio ya kundi hilo lililokuwa dhidi ya mapinduzi. Kusimama kidete mtaa kwa mtaa wananchi wa mji wa Amol dhidi ya mashambulio ya kundi hilo kumeufanya mji wa Amol utambulike na kuwa mashuhuri kwa jina la mji wa ngome elfu moja.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani, Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu.
Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".