Jumapili tarehe 6 Februari 2022
Leo ni Jumapili tarehe 4 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 6 Februari 2022.
Miaka 851 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiislamu, Muhammad ibn Ali al-Wasiti maarufu kwa jina la Ibn Muallim. Alizaliwa mwaka 501 Hijiria. Mashairi ya malenga huyo yalibeba ujumbe wa maadili na tabia njema na masuala mengine ya kijamii kwa kutumia lugha nyepesi. Baadhi ya mashairi ya Ibn Muallim yanahusiana na masuala ya kiroho na kiirfani. Athari pekee ya Ibn Muallim ni kitabu cha tungo za mashairi ya malenga huyo.

Siku kama ya leo miaka 405 iliyopita alifariki dunia daktari na mtaalamu wa mimea wa Italia, Prospero Alpini. Alizaliwa mwaka 1553 na baada ya kuhitimu masomo ya tiba alitunukiwa shahada ya udaktari. Katika uchunguzi na utafiti wake, Prospero Alpini aligundua kwamba, mimea kama walivyo wanyama, ina jinsia mbili za kike na kiume japokuwa hakuweza kujua kama kanuni hiyo inahusu kila kitu.
Miongoni mwa hatua nyingine muhimu za Prospero Alpini ni kuarifisha kahawa na ndizi kwa watu wa Ulaya. Biashara ya kahawa ya Mocha au al Mukha ambalo ni jina la bandari iliyoko kusini mwa Yemen, ilikuwa mikononi mwa Waislamu tangu karne ya 15, na mtaalamu huyo wa mimea wa Italia ndiye aliwajulisha watu wa Ulaya aina hiyo ya kahawa (Arabica) iliyokuwa ikioteshwa katika maeneo ya milimani nchini Yemen.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo. Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani.

Miaka 86 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo. Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri.

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili, alimu na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria katika eneo la Jabal Amili nchini Lebanon na kupata elimu ya msingi ya Kiislamu nchini humo. Ayatullah Sayyid Amin alielekea Najaf nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 24 kwa shabaha ya kukamilisha elimu ya juu na kupata elimu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Baadaye alielekea Syria na kutoa huduma kubwa za kufundisha Uislamu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi muhimu zaidi kikiwa kile cha A'yanul Shia chenye juzuu kumi. Katika kitabu hicho Sayyid Muhsin al Amin amearifisha vinara wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia hususan maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na mchango wao katika kuimarisha ustaarabu wa Kiislamu. Kitabu kingine cha msomi huyo ni Kashful Irtiyab fii Atba'I Muhammad bin Abdul Wahhab kinachofichua na kukosoa itikadi za kundi potofu la Kiwahabi.

Tarehe 6 Februari miaka 59 iliyopita aliaga dunia mwanaharakati mashuhuri na mpigania uhuru wa Morocco Abd-el Karim Al-Khattabi. Alianzisha harakati za kupambana na wakoloni wa Kihispania na Kifaransa akiwa bado kijana na kuunda kundi la mapambano katika maeneo ya milimani nchini humo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia Uhispania ilifanya mauaji mengi ya halaiki huko Morocco kwa ajili ya kupanua mamlaka na ushawishi wake. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na wakati wa kupamba moto mapambano ya wanamapinduzi wa Morocco, Ufaransa nayo ilifanya mauaji dhidi ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo.

Na siku kama hii ya leo miaka 43 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini baada ya kutangazwa serikali ya muda ya Mapinduzi. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Katika siku hiyo pia wananchi wa Iran na kwa sauti moja walitaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu. Siku hiyo pia Jenerali Robert Ernest Huyser, mjumbe maalumu wa Marekani aliyekuwa Tehran kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuubakisha madarakani utawala wa Shah Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa makamanda wa jeshi la Shah, alifunga virago na kurejea Marekani baada ya kushindwa kusitisha wimbi la Mapinduzi ya Kiislamu.
