Feb 06, 2022 23:07 UTC
  • Jumatatu, Februari 7, 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 5 Rajab 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Februari 2022 Milaadia.

Tarehe 5 Rajab miaka 1199 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."

Siku kama ya leo miaka 544 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza. Mwanzoni More alisomea elimu ya sheria na baada ya kujiunga bungeni akapewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo. Hatimaye More akanyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 Miladia akiwa na umri wa miaka 57.

Thomas More

Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na fasihi wa nchini Uingereza. Awali Browne alisomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake kusoma tamaduni za mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Aidha mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa njia bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairan kuelekea maeneo mengine ya dunia. Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, na kufariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54.

Edward Granville Browne

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, sawa na tarehe 7 Februari 1999, alifariki dunia Hussein bin Twalaal, mfalme wa zamani wa Jordan kutokana na maradhi ya saratani. Mfalme Hussein alizaliwa 1935 mjini Amman, na kupata elimu yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Uingereza. Mfalme Hussein alichukua wadhifa wa ufalme wa Jordan mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 17 baada ya kuuawa babu yake Mfalme Abdullah, na utawala kukabidhiwa baba yake Twalaal ambaye naye alitawala kwa miezi michache tu. Mfalme Hussein alikuwa muitifaki wa karibu wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, na ilifikia hatua ya kutia saini makubaliano ya amani na Wazayuni mwaka wa 1994.

Hussein bin Twalaal

Na siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Februari 1974, nchi ndogo ya Grenada iliyoko Amerika ya Latini ilijipatia uhuru wake. Nchi hiyo iliyoko kisiwani, ilivumbuliwa mwaka 1498 na mvumbuzi mashuhuri wa Kihispania Christopher Columbus. Amma baada ya kutokea sutafahumu kati ya nchi za Uhispania, Ufaransa na Uingereza juu ya umiliki wa kisiwa hicho, hatimaye Ufaransa iliidhibiti na kuitawala nchini hiyo mwaka 1674. Baada ya kupita karibu karne moja, mnamo 1783, Waingereza waliikoloni nchi ya Grenada kwa muda wa karne mbili, na hatimaye mwaka 1974 katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru wake.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, muwafaka na tarehe 18 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wananchi wa Iran kama ilivyokuwa siku kadhaa zilizopita, walijitokeza makundi kwa makundi kwa shabaha ya kuonana na Imam Khomeini kwenye makaazi yake mjini Tehran, na kutangaza utiifu wao kwa shakhsia huyo. Licha ya wananchi wa kawaida kutoka matabaka mbalimbali, makundi kadhaa ya wanajeshi huku wakiwa wamevalia sare za kijeshi, walikwenda kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini (M.A).