Jumanne tarehe 8 Februari 2022
Leo ni Jumanne tarehe sita Rajab 1443 Hijria sawa na Februari 8 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 960 iliyopita Hassan as-Sabbah mmoja wa viongozi wakubwa wa Waislamu wa Shia Ismailiyah, alitwaa udhibiti wa ngome muhimu na imara ya Alamut, iliyo karibu na mji wa Qazvin, kaskazini mwa Iran. As-Sabbah ambaye kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hapo alikuwa akiwalingania watu kumfuata yeye, aliimarisha utawala wake baada ya kutwaa udhibiti wa ngome hiyo ambapo muda punde baadaye alipata kudhibiti miji mingine pia. Aidha baada ya kudhibiti ngome hiyo ya Alamut, kuliongezeka tabligh (linganio) za kuwataka watu wajiunge na madhehebu ya Shia Ismailiya na wafuasi wa wake walifanya mauaji dhidi ya viongozi wa utawala wa Seljuqi, akiwemo Khoja Nidham al-Mulk. Ngome ya Alamut iliendelea kuwa tegemeo la wafuasi wa Ismailiya nchini Iran hadi pale ilipoangukia mikononi mwa utawala wa Hulagu Khan mwaka 654 Hijiria. Hassan as-Sabbah alifariki dunia mwaka 518 Hijiria.
Tarehe 6 Rajab miaka 927 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq. Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima.

Tarehe 8 Februari miaka 59 iliyopita Kanali Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa kijeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah. Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakijibu wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi. Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran huku vikiwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Khomeini. Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani. Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.