Feb 10, 2022 01:02 UTC
  • Alkhamisi tarehe 10 Februari 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Rajab 1443 Hijria inayiosaidfiana na tarehe 10 Februari 2022.

Tarehe 8 Rajab miaka 410 iliyopita alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa zama hizo hususan katika elimu za fiqhi na Hadithi. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwao ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Ummah. Mwanazuoni huyo aliaga dunia mwaka 1114 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 259 iliyopita ulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa katika mji wa Paris. Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada. Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika kipidi hicho Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya, na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita alifariki dunia Sophia Krukovsky mwanahisabati wa Russia. Alizaliwa mwaka 1850 mjini Moscow. Licha ya kuwa alipendelea sana elimu ya hisabati, lakini kutokana na sababu za kibaguzi hakuweza kujiunga na chuo kikuu na ni kwa msingi huo ndio maana akaelekea nchini Ujerumani na kujifunza elimu ya hisabati na fizikia. Pamoja na hayo Sophia Krukovsky alikabiliwa na matatizo mengi kabla ya kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Kufuatia hali hiyo alilazimika kusoma elimu hiyo kwa mwalimu wa hisabati nje ya chuo kikuu. Mwaka 1874 Sophia Krukovsky alitunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) bila kuhudhuria chuoni. Aidha mwaka 1888 alitunukiwa zawadi yenye itibari katika chuo cha academia nchini Ufaransa. Kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1891 alipofariki dunia alijishughulisha na kazi ya ufundishaji wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden.

 Sophia Krukovsky 

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani. Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru.

Siku kama ya leo miaka  72 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "Mc Carthisim" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya Mc Carthisim ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.

Joseph Mc Carthy

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo.

Savak