Jumamosi, Februari 12, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 10 Rajab 1443 Hijria mwafaka na tarehe 12 Februari 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar. ***

Siku kama ya leo miaka 1248 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi Al-Jawad AS alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS. Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui." ***

Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza, Charles Darwin. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu namna ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu. Baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa. ***
Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita nchi ya Chile ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Chile ilikaliwa kwa mabavu na Uhispania mnamo mwaka 1536. Mwaka 1788, Mfalme Charles III aliyekuwa mfalme wa Uhispania aliangalia upya makoloni yake na hivyo akaamua kuikabidhi nchi hiyo kwa Peru. Harakati ya kwanza ya kupigania uhuru nchini Chile ilianza mwaka 1814 Miladia. Katika harakati hizo wapiganaji waliokuwa wanataka kujitenga walishindwa vibaya na askari wa serikali ya kikoloni. Hata hivyo mwaka 1817 Miladia, José de San Martín, raia wa Argentina akishirikiana na maelfu ya wapiganaji alianzisha harakati dhidi ya makoloni ya Mfaransa ikiwemo Peru na Chile. Kwa uungaji mkono wa raia wa Chile hatimaye alifanikiwa kuwatimua wakoloni wa Uhispania na nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1818 Miladia. ***
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita aliuawa shahidi mwasisi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na mwanamapambano mashuhuri wa Misri, Ustadh Hassan al Banna. Hassan al Banna aliuawa shahidi katika njama iliyopangwa na Uingereza kwa kushirikiana na Mfalme Faruq wa Misri. Alianza mapambano yake dhidi ya ukoloni na vibaraka wake akiwa chuo kikuu ambapo alianzisha harakati ya kupambana na sera za kupinga dini ya Kiislamu za Uingereza kwa kuasisi hatakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 1928. Harakati hiyo ilikuwa kwa kasi na kuenea katika nchi za Syria, Jordan, Lebanon, Palestina na katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika. Serikali ya Misri ilipiga marufuku harakati ya Ikhwanul Muslimin mwaka 1948 na kuwatia jela wanachama wake wengi na kisha kumuua shahidi kiongozi wake Sheikh Al Banna. ***
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu. ***
Na tarehe 12 Februari miaka 14 iliyopita aliuawa shahidi Imad Mughnia maarufu kwa jina la Haj Ridhwan, ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulizi la kigaidi lililofanyika mjini Damascus, Syria. Kamanda Mughnia aliuawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa na vibaraka wa Israel katika gari lake. Shahid Mughnia alijiunga na harakati za mapambano baada ya uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Baadaye kidogo alijiunga na harakati ya Hizbullah na kushika nyadhifa za juu katika harakati hiyo. Shahid Mughnia alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Hizbullah dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya utawala huo nchini Lebanon mwaka 2006. ***