Feb 13, 2022 01:10 UTC
  • Jumapili tarehe 13 Februari 2022

Leo ni Jumapili tarehe 11 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 13 Februari 2022.

Miaka 1172 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa mjini Baghdad mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn al Anbari. Alijifunza elimu ya Hadithi baada ya kukamilisha masomo yake ya lugha na sayansi za Qur'ani tukufu. Ibn al Anbari alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuhifadhi na kushika vitu kichwani mwake. Alikwua mtu mwema na mchamungu saba  na mbali na kujishughulisha na kufundisha na kuklea vizzi vya maulamaa  mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya "Adabul Kaatib" na "Dhamaairul Qur'ani." Alifariki dunia mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57.

Miaka 872 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa Hadithi Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata elimu katika vituo vya kielimu vya Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimishqi."

Siku kama ya leo mwaka 1945 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani. Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani. 

Miaka 34 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani. Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr hapa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake. Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake mjini Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chimbuko la uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa. Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu.

Ayatullah Sheikh Salman Khaqani