Feb 15, 2022 23:04 UTC
  • Jumatano, Februari 16, 2022

Leo ni Jumatano tarehe 14 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 16 Februari 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita baina ya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina, yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa pili ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maquraish. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Bendera ya Lithuania

Siku kama leo miaka 76 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya Zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1992 aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi