Jumamosi, 19 Februari, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 17 Rajab 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 19 Februari 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 549 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus. Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. ***
Miaka 322 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe tarehe 17 Rajab, alifariki duani Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kishia. Sheikh Abul-Hassan Sulaiman Ibn Abdillah Ibn Ali Ibn Hassan Bahrani Mahuzi, maarufu kwa jina la Muhaqqiq Bahrani, mmoja wa maulama wa Kishia wa mwanzoni mwa karne ya 12 Hijiria, alizaliwa katikati ya mwezi wa Ramadhani mwaka 1076 Hijiria. Alibobea katika elimu ya hadithi, wapokezi wa hadithi, historia na maisha ya mtukufu Mtume (saw) na Ahlu Baiti wake (as). Sheikh Abdullah Samahiji na Sayyid Hashim Bahrani, mwandishi wa tafsiri ya Qur'an ya Al-Burhan na Sheikh Ahmad Bahrani, ni miongoni mwa wanafunzi wa Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'al-Shifaau fil-Hikmat al-Nadharia wal-Mi'raaj.' Msomi huyo mkubwa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 46. ***
Katika siku kama ya leo miaka 172 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, Sayyid Abu-Turab Khansari, mmoja wa maulama na maustadhi wakubwa alizaliwa huko Khansar moja ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullahil Udhma Khansari alisoma masomo ya akili na nakili kwa maustadhi muhimu wa zama zake. Juhudi zake masomoni zilimfanye aondokee kuwa ustadhi mahiri katika masomo ya fiqhi, usulul fiqhi na tafsiri ya Qur'ani. Ayatullah Khonsari ameandika vitabu vingi kuhusiana na elimu mbalimbali za kidini. Kitabu cha Qasdus Sabil kuhusiana na elimu ya usulul fqhi na Misbahus Swalihiin kinachozungumzia misingi ya dini, ni baadhi tu ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyu mahiri wa Kiislamu aliyefariki dunia mwaka 1346 Hijria. ***
Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Februari mwaka 1951 alifariki dunia mwandishi na mkosoaji mashuhuri wa Ufaransa akiwa na umri wa miaka 82. Alizaliwa mwaka 1869 Miladia mjini Paris lakini alitumia umri wake mwingi Afrika kaskazini na hasa nchini Algeria. Visa vingi alivyoandika viliathiriwa na maisha pamoja na utamaduni wa watu bara hilo. Miongozi mwa visa vya kuvutia vilivyoandikwa na mwandishi huyo ni pamoja na "Wimbo wa kijijini" na "Meza ya Ardhi." Mwaka 1947 Gide alitunukiwa zawadi ya Nobel. ***
Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1952 alifariki dunia mwandishi wa Norway, Knut Hamsun. Alizaliwa mwaka 1859 katika familia masikini kaskazini mwa nchi hiyo, na alipotimiza miaka 24 aliingia katika uwanja wa uandishi. Hamsun alisafiri mara mbili kwenda Marekani na akaandika makosa aliyoyaona nchini humo ndani ya kitabu alichokipa anwani ya "Maisha ya Kimaanawi katika Zama Mpya Nchini Marekani" pia aliandika kitabu kilichopewa jina la "Njaa" ambacho kilibeba tamaduni mbali mbali za dunia. Uandishi wake wa kitabu cha "Matunda ya Ardhini" ulikuwa na nafasi muhimu katika kutunukiwa zawazi ya Nobel mwaka 1920. ***
Na miaka 12 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi. Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki. Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo. ***