Jumamosi, 26 Februari, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 24 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 26 Februari 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1103 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu. ***
Miaka 231 iliyopita katika sikuu kama ya leo alifariki dunia Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf. Akiwa mjini hapo haraka alifikia daraja ya umarjaa sambamba na kuteuliwa kuwa mkuu wa hauzana chuo kikuu cha kidini cha mji huo mtakatifu. Alifanya mabadiliko katika chuo hicho kikongwe. Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’hab ya Kishia. Aidha aliwalea wanafunzi wengi, bila kusahau kazi ya kufafanua vitabu. Maulama kama vile Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa, Mulla Ahmad Naraqi, Muhammad Baqir Shafati, Sayyid Muhammad Jawad Aamili…ni baadhi ya wanafunzi wa Sayyid Bahrul-Ulum. Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo. ***
Tarehe 26 Februari miaka 220 iliyopita yaani mwaka 1802 alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo. Alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25. Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki mwaka 1885. ***
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia, mvumbuzi wa Marekani kwa jina la Richard Jordan Gatling. Getling alizaliwa mwaka 1818 na katika umri wake alivumbua vitu kadhaa moja wapo ikiwa ni bunduki iliyopewa jina lake ya Getling. Bunduki ya Getling ina mabomba kadhaa ambayo baada ya ufyatuaji kila moja huzunguka na kuachia risasi kwa hatua, na kuipa uwezo wa kufyatua risasi nyingi kwa wakati mmoja. Mzunguko wa mabomba hayo ulitengenezwa na Richard Jordan Gatling mwenyewe. ***
Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, yaani mwaka 1921 kulisainiwa mkataba wa kirafiki baina ya Iran na Urusi ya zamani. Katika mkataba huo ambao ulisainiwa baada ya miaka minne ya mapinduzi ya Muungano wa Sovieti ya zamani, Moscow ilitangaza kwamba, haingeendelea na siasa za kikoloni dhidi ya Iran zilizokuwa zikifuatwa na utawala wa Tzar nchini humo. Kwa mujibu wa kifungu hicho muungano huo wa zamani uliacha kutekeleza mikataba ya awali iliyokuwa inaidhuru Iran. Katika mkataba huo wa urafiki Moscow ilitangaza kwamba haingetambua tena mikataba yote iliyotiwa saini na utawala wa tatu wa Tzar dhidi ya Iran. Hata hivyo Urusi ya zamani haikuipatia Iran ardhi za Caucasia na Turkmenistan zilizopo kaskazini magharibi na mashariki mwa Iran. Aidha katika mkataba huo Iran iliahidi kutoruhusu nchi nyingine kutumia ardhi yake dhidi ya Urusi. Itakumbukwa kuwa, Urusi kipindi hicho ilikuwa inakabiliwa na vitisho vya nchi za Magharibi. ***
Miaka 66 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5. Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda. ***
Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita sawa na tarehe 7 Isfand 1377 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji ulifanyika katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa muktadha huo kukawa kumefikiwa moja ya lengo jingine miongoni mwa malengo matukufu ya taifa la Kiislamu la Iran. Kwa kufanyika uchaguzi huo kwa hamasa, asasi na ngome ya wananchi ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji katika uga wa kiutawala ikawa imepata dhihirisho la kivitendo. Kuundwa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji zaidi ya 33,000 katika maeneo mbalimbali ya Iran, ikawa ni hatua moja mbele katika uga wa kuingia na kuweko ushiriki wa wazi wa wananchi wote katika uchukuaji maamuzi ya nchi. ***
