Jumanne tarehe Mosi Machi 2022
Leo ni Jumanne tarehe 27 Rajab 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Machi 2022.
Siku kama ya leo miaka 1456 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (saw) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (saw) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alitumia muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumwambia kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake wa Mwisho kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanaadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Siku kama ya leo miaka 976 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za Hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".
Katika siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Tarehe 10 Esfand miaka 43 iliyopita hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 15. Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko. Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza harakati ya Mapinduzi.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza. Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW). Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa hususan barani Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo na kutangaza mafundisho sahihi ya Uislamu. Matangazo ya IRIB pia yananawabaishia Walimwengu ubeberu wa Marekani na madola ya Kimagharibi dhidi ya mataifa mengine na ukandamizaji wa utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.