May 30, 2016 06:00 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 30

Real Madrid wakishangilia baada ya kutwaa Kombe la UEFA

Voliboli: Iran yaizaba Canada mashindano ya kufuzu Olimpiki ya Rio

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kung'ara katika michuano ya kutafuta tiketi ya kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Rio inayoendelea huko Tokyo, Japan. Katika mchuano wa Jumapili uliopigwa katika ukumbi wa Tokyo Metropolitan Gymnasium, timu hiyo ya wanaume ya Iran iliitandika Canada seti 3-2 za (27-29, 19-25, 25-20, 25-21, 16-14).

Siku ya Jumamosi, Iran iliichabanga Australia seti 3-0 ikiwa ni siku ya kwanza ya mashindano hayo ya kuwania kutinga Olimpiki ya Rio de Jeneiro nchini Brazil mwezi Agosti mwaka huu. Timu hiyo ya voliboli ya wanaume ya Iran inatazamiwa kuvaana na Ufaransa Jumanne hii. Mashindano ya Olympic Qualification Tournament yanayopigwa huko Tokyo Japan yalianza Mei 28 na yanatazamiwa kufunga pazia lake Juni 5.

Soka Afrika

Kenya yatoka sare na Tanzania mchuano wa kirafiki

Timu ya taifa ya soka ya Kenya imelazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchuano wa kirafiki uliopigwa katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi Jumapili. Vijana wa Taifa Stars wakiwa ugenini, walifanikiwa kufunga goli la uongozi kunako dakika ya 33 kupitia kwa mshambuliaji wake anayeichezea klabu ya Stand United, Elias Maguli, ambaye katika Ligi Kuu ya Tanzania bara amefanikiwa kufunga magoli 14.

Hata hivyo furaha ya Taifa Stars ya Tanzania ambayo inajiandaa kwa mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON dhidi ya timu ya taifa ya Misri Juni 4 katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ilikatizwa dakika tano baadaye, baada ya Harambee Stars kufanya mambo kuwa 1-1, kupitia mkwaju wa penati uliopigwa na nahodha wa timu hiyo ambaye pia anayeichezea klabu ya Southampton ya Uingereza, Victor Wanyama. Hii ni baada ya kiungo Ayub Timbe kuchezewa visivyo na Mtanzania Ramadhan Shiza katika sanduku la hatari.

TFF kutoandaa Kagame Cup mwaka huu

Shirikisho la Soka la Tanzania TFF limesema halitakuwa katika nafasi ya kuandaa michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA. TFF ilikuwa imeahidi kuchukua nafasi ya Zanzibar iliyopewa jukumu hilo lakini ikajiondoa kutokana na kile kilochotajwa kuwa sababu za kifedha. Rais wa TFF Jamal Malinzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter amesema: "Nchi yake haitaweza kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa sababu ya msongamano wa mechi za kimataifa jijini Dar es Salaam baada ya Yanga FC kufuzu kucheza hatua ya makundi kuwania taji la Shirikisho." Michuano hiyo ambayo inafahamika kama Kagame Cup imepangwa kufanyika kuanzia katikati ya mwezi wa Julai hadi mwanzoni mwa mwezi wa Agosti. Mwaka 2015 michuano hii ilifanyika nchini Tanzania na wenyeji Azam FC wakanyakua ubingwa kwa kuwachachawiza vijana wa Gor Mahia ya Kenya mabao 2 kwa 0 katika fainali. Tanzania imewahi kuandaa michuano hii mara tatu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku Kenya ikiandaa michuano hii mara ya mwisho mwaka 2001.

Real Madrid yatwaa Kombe la UEFA

Klabu ya Real Madris imetwaa kutwaa ubingwa wa msimu huu wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League kwa mara ya 11. Hii ni baada ya klabu ya Real kuwalaza watani wao wa mjini Atletico Madrid mabao 5-3 kupitia mikwaju ya penalti. Usiku wa Ijumaa ya Mei 28, wapenda soka wote duniani macho na masikio yao ilikuwa ni katika uwanja wa San Siro katika jiji la Milan nchini Italia, ili kutaka kufahamu nani atafanikiwa kuchukua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya 2016 kati ya Real Madrid na Atletico Madrid. Timu hizo ziliingia katika mikwaju ya penati baada ya kumalizika dakika 90 za kawaida na 30 za ziada za mchezo kwa sare ya goli 1-1. Goli la Real lilipachikwa kimyani na kiungo nyota Sergio Ramos katika dakika ya 15. Bao la kusawazisha mambo la Atletico lilifungwa na Ferreira Carrasco katika dakika ya 79 ya mchezo. Furaha, nderemo, shangwe na vigelegele vilitawala kwenye uwanja wa San Siro mjini Milan miongoni mashabiki na wachezaji wa Real Madrid mwishoni mwa wiki hii.

Msimu huu wa mwaka 2016 umeonekana kuwa nuksi kwa vijana wa Atletico kutokana na kutofanikiwa kuweka rekodi ya kutwaa Kombe hilo kwa mara ya kwanza, lakini kwa upande wa Real Madrid hilo linakuwa Kombe lao la 11 la Klabu Bingwa Ulaya. Ilikuwa furaha isiyo na kifani kwa mkufunzi mpya wa klabu hiyo Zinedine Zidane, ambaye kibarua chake cha kwanza katika klabu hiyo kilikua ni kuhakikisha kuwa vijana wake wanaibuka mabingwa.

Dondoo: Madaktari bingwa na WHO watofautiana kuhusu Olimpiki ya Rio

Ikiwa imesalia takriban miezi mitatu kufanyika Mashindano ya Olimpiki ya Rio, mashindano hayo ya kimataifa yameingia doa baada ya madaktari bingwa 150 duniani pamoja na wataalamu wa maswala ya afya kuungana pamoja kupinga mashindano kufanyika kutoka na virusi vya Zika nchini Brazil. Madaktari hao wamependekeza mashindano hayo yaahirishwe kwa sasa mpaka kutakapokuwa na usalama wa kiafya nchini humo au yafanyike sehemu nyingine tofauti na Brazil. Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Afya Dunia WHO limepinga mpango wowote wa kuahirisha, kuhamishwa au kusogeza mbele mashindano hayo ya kimataifa. Dakta Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema shirika hilo limehakikishiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kuwa mikakati yote ya kiafya ya kuhakikisha kuwa wanaokwenda kushiriki au kutazama mashindano hayo hawaambukizwi.

………………………TAMATI………………… 

 


Tags