Ijumaa tarehe 4 Machi 2022
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe 4 Machi 2022.
Mwezi wa Shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake wamewausia mno Waislamu kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Siku kama ya leo miaka 750 iliyopita Ghiathuddin Abu Madhaffar Abdul Karim bin Ahmad anayefahamika kwa lakabu ya Ibn Taus, alifariki dunia huko Kadhimain, moja kati ya miji ya Iraq. Ibn Taus alikuwa faqihi na mwandishi mashuhuri wa karne ya saba Hijria. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kiarabu na kupata elimu kwa wanzuioni wakubwa kama Khajah Nasiruddin Tusi. Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.

Tarehe 4 Machi miaka 199 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu elfu 12 wakati wa vita vyao dhidi ya jeshi la ufalme wa Othmania katika mji wa Tripolitsa. Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya utawala wa Kiothmani yaliamua kulipiza kisasi kwa kuua kundi la Wagiriki.
Tarehe Mosi Shaabani miaka 177 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahibul Jawahir. Sahibul Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo. Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na umakini mkubwa.
Na katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita mji wa Herat ulioko kaskazini-magharibi mwa Afghanistan ya sasa ulijitenga na Iran. Mji huo na maeneo ya jirani yalikuwa sehemu ya Irani. Baada ya kupanuka ushawishi na uwepo wa Waingereza katika Bara Hindi, nchi hiyo ilichochea kujitenga kwa Herat na Iran na baadaye watawala wa Kabul na Kandahar walilivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la Herat.