Mar 06, 2022 02:43 UTC
  • Jumapili tarehe 6 Machi 2022

Leo ni Jumapili tarehe 3 Shaabani 1443 Hijria sawa na tarehe 6 Machi 2022.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka. Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka. Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayah hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu. Aidha akiwa mjini Makka Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo. Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa.

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita alizaliwa Ayatullah Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya kati alielekea Najaf, Iraq na kupata elimu kwa maulama wakubwa wa zama. Alifikia daraja ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 26 na baada ya kurejea Isfahani alijikita katika shughuli ya kufundisha sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake wavue vazi la staha la hijabu, Ayatullah Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.

Ayatullah Hussein Khadimi

Miaka 122 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.

Gottlieb Daimler

Siku kama ya leo, miaka 85 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia. Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege. Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6.

alentina Tereshkova

Tarehe 6 Machi miaka 65 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.

Bendera ya Ghana

Na siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Machi 1975, yalitiwa saini makubaliano ya kuzitafutia ufumbuzi hitilafu baina ya Iran na Iraq huko Algiers, mjimkuu wa Algeria. Makubaliano hayo yalifanyika kufuatia mazungumzo baina ya Mfalme wa Iran na Rais wa wakati huo wa Iraq dikteta Saddam Hussein. Kwa mujibu wa mkataba huo ambao unajulikana pia kwa jina la mkataba wa 1975, Iran na Iraq ziliafikiana juu ya kuanishwa mipaka ya ardhini na majini.

 

Tags