Mar 10, 2022 22:59 UTC
  • Ijumaa tarehe 11 Machi  2022

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Shaabani 1443 Hijria sawa na Machi 11 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1118 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu. Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni.

Siku kama ya leo miaka 881 iliyopita alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa Hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza pia elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya awali alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz. Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau na kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Haj Hussein Khadimi alizaliwa mjini Isfahani, Iran mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi. Akiwa na umri wa miaka 26 alifikia daraja ya ijtihadi ambapo baada ya kurejea mjini Isfahani alijikita na shughuli ya ufundishaji sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi ambapo alikuwa na wanafunzi wengi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake kutovaa hijabu Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.

Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita yaani mwaka 2004, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa kufuatia miripuko 5 ya mabomu iliyotokea kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid, Uhispania. Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia. Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo ililituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika katika miripuko hiyo. Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Kisoshalisti kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq.

Tarehe 11 Machi mwaka 2006 dikteta wa zamani wa Yugoslavia, Slobodan Milosevic akiwa na umri wa miaka 64 alifariki dunia ndani ya jela katika mji wa the Hague. Miezi 9 baada ya kuanguka utawala wake mwaka 2001, Milosevic alitiwa mbaroni na kukabidhiwa kwenye mahakama ya uhalifu wa kivita ya Hague. Akiwa kijana alijiunga na chama cha kikoministi cha Yugoslavia ya zamani. Mwaka 1989 Milosevic akawa Rais wa Serbia. Milosevic aliongoza vita vilivyoanza mwaka 1992 na kuendelea kwa muda wa miaka mitatu na nusu dhidi ya watu wa Bosnia Herzegovina. Katika vita hivyo Waislamu wa Bosnia laki mbili waliuawa, huku wengine milioni 2 wakilazimika kukimbia makazi yao. Kufuatia kushindwa kwa Slobodan katika uchaguzi mwaka 2000 na kushadidi upinzani wa ndani dhidi yake, hatimaye utawala wake ulianguka na baada ya muda alitiwa mbaroni. Kesi ya Milosevic ilianza kusikilizwa mwaka 2002, hata hivyo kifo chake kilitokea kabla ya kumalizika kesi hiyo.

Slobodan Milosevic

Na miaka 11 iliopita katika siku kama ya leo yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa daraja 9 kwa kipimo cha Rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan. Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa kwa watu elfu 12 na malaki kadhaa ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo halijawahi kutokea mfano wake tangu makumi ya miaka yaliyopita nchini humo. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda kadhaa Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.