Mar 14, 2022 02:52 UTC
  • Jumatatu tarehe 14 Machi 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Shaabani 1443 Hijria sawa na Machi 14 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1410 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake, Mtume Mtukufu (saw), alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake, Imam Ali (as), na baba yake, Imam Hussein (as). Ali bin Hussein alikuwa maarufu kwa jina la Ali al Akbar yaani Ali Mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma za utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana.

Siku kama ya leo miaka 914 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.

Sanai Ghaznawi

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Machi 1879 alizaliwa Albert Einstein, msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati nchini Ujerumani. Mnamo mwaka 1921 msomi huyo alipewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia, baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti. Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia zilikuwa na taathira kubwa duniani. Hata hivyo Einstein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba uchunguzi na utafiti wake katika uwanja wa atomu umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia. Albert Einstein alifariki dunia 1955.

Albert Einstein

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani, mmoja wa maulama wachaji-Mungu wakubwa na mwanamapambano. Alizaliwa mwaka 1262 Hijiri mjini Isfahan, Iran. Baba na babu yake, walikuwa kati ya maulama wakubwa wa eneo ambapo naye pia alipata kusoma kutoka kwao elimu mbalimbali. Baada ya Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani kusoma baadhi ya masomo ya kidini kutoka kwa baba yake (yaani Muhammad Baqir Agha Najafi) alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo mjini hapo. Miaka mitano baadaye alirejea mjini Isfahan na kuwa mmoja wa maraajii wakubwa wa mji huo. Aidha mbali na masuala ya kidini, Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani alikuwa mwanaharakati mzuri wa masuala ya kisiasa. Katika uwanja huo, msomi huyo alipambana vikali na upotoshaji wa kifikra na kiutamaduni na kadhalika ufisadi wa watawala dhalimu wa wakati huo. Wakati huo huo aliongoza harakati za kimapambano dhidi ya ukoloni wa kigeni hususan Uingereza. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Fiqhul-Imaamiyyah' 'Bahth Fii Wilaayati Haakimul-Faqih' na 'Dalaailul-Ahkam.'

Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani

Miaka 68 iliyopita yaani mnamo mwaka 1954 tarehe 14 mwezi Machi vilianza vita vya kihistoria na vikubwa vilivyojulikana kwa jina la vita vya" Dien Bien Phu" ambavyo viliainisha mustakbali wa wanajeshi wa kikoloni wa Ufaransa huko Indochina. Katika vita hivyo wapiganaji wa harakati ya wanamapinduzi ya Viet Minh waliokuwa wakipigania ukombozi wa Vietnam walipambana na jeshi la wakoloni wa Kifaransa waliokuwa katika ngome ngumu kudhibitiwa ya Dien Bien Phu. Hatimaye tarehe 7 Mei mwaka huo huo vita hivyo vilifikia tamati kwa kusalimu amri kamanda wa majeshi ya Ufaransa aliyekuwa katika ngome ya Dien Bien Phu. Vita hivyo viliwafungisha virago wakoloni wa Ufaransa nchini Vietnam.

Vita vya Dien Bien Phu

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita,  yaani tarehe 14 Machi 1978, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kuivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv. Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon. Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano shupavu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo. 

Uvamizi wa Israel huko Lebanon

 

Tags